Mufindi FM
Mufindi FM
16 June 2026, 8:12 pm

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Mhe. Dkt. Linda Salekwa akihutubia katika maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika kiwilaya katika shule ya msingi Imehe. Picha na Kelvin Ayoub.
Chimbuko la siku hiyo ya mtoto wa Afrika ni mauaji ya kinyama ya watoto wa shule yaliyotokea tarehe 16 Juni, 1991 katika kitongoji cha Soweto nchini Afrika kusini na ilianzishwa na Umoja wa Afrika (AU) kwa lengo la kuenzi ujasiri wa watoto hao na ustawi wa haki zao kote barani Afrika.
Na Kelvin Ayoub
Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Dkt. Linda Salekwa amewataka wazazi na walezi kuwajibika katika malezi ya watoto na kuhakikisha wanawalinda dhidi ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji ili kujenga familia bora na Taifa imara.
Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Mtoto Afrika yaliyofanyika Juni 16, 2026 katika Shule ya Msingi Imehe, iliyopo wilayani hapo. Mkuu huyo Dkt. Salekwa amesema watoto wanahitaji kulelewa katika misingi ya maadili mema huku akisisitiza kuwa nao wanapaswa kuwajibika katika kufuata malezi wanayopewa na wazazi na walezi wao.
Sauti DC Salekwa
Aidha, amewapongeza wadau wa maendeleo wa Wilaya ya Mufindi wakiwemo World Vision, RDO, SOS na CAMFED kwa mchango wao katika utekelezaji wa miradi na huduma zinazowanufaisha watoto na jamii kwa ujumla.

Mkuu wa wilaya ya Mufindi Mhe. Dkt. Linda Salekwa akiwa na wanafunzi katika maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika kiwilaya yaliyofanyika katika shule ya msingi Imehe iliyopo Nyololo wilaya humo. Picha na Kelvin Ayoub.
Dkt. Salekwa pia amewataka wazazi kuacha kuruhusu migogoro yao binafsi kuwaathiri watoto, akisisitiza kuwa watoto hawapaswi kuumizwa au kunyimwa haki zao kutokana na tofauti za wazazi.
Sauti DC Salekwa migogoro
Sambamba na hilo, pia Dkt. Linda Salekwa amekabidhi magodoro 160, vitanda 80, viti 150 na meza 150 vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 38 vilivyotolewa na Shirika la World Vision kupitia Nyololo Area Program (AP),vifaa hivyo Katika Shule ya Sekondari Nyololo na Shule ya Sekondari Kihenzile huku akiwataka walimu na wanafunzi kuvitunza ili viweze kuendelea kusaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Pichani ni miongoni mwa msaada wa vitanda 80 vilivyotolewa na shirika la World Vision kupitia Nyololo Area Program (AP) katika maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika kiwilaya katika viwanja vya Shule ya Msingi Imehe, iliyopo wilayani Mufindi. Picha na Kelvin Ayoub.
Kwa upande wake, Mwezeshaji wa World Vision Nyololo AP Bw. Humphrey amesema shirika hilo linaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu ulinzi wa mtoto na kupinga vitendo vya ukatili ili kuhakikisha watoto wanakua katika mazingira salama.
Sauti Mwezeshaji World Vision
Naye Mratibu wa Mradi wa Nyololo AP Bw. Joseph Shayo amesema msaada huo umetolewa kwa lengo la kuboresha mazingira ya watoto kujifunzia na kuimarisha malezi bora, huku shirika hilo likiendelea kushirikiana na serikali katika kulinda na kuendeleza ustawi wa mtoto.
Sauti Mratibu Mradi wa AP Nyololo
Nao baadhi ya wanufaika wa miradi ya World Vision wameeleza kuwa msaada na mafunzo yanayotolewa na shirika hilo yamechangia kuboresha maisha ya familia nyingi kupitia miradi ya lishe, elimu, afya na uwezeshaji wa kiuchumi, huku wakilishukuru shirika hilo kwa kuendelea kuwa karibu na jamii.
Sauti Wanufaika
Maadhimisho hayo yaliambatana na utoaji wa zawadi mbalimbali kwa watoto ikiwemo zaidi ya lita 80 za maziwa, mafuta ya kupikia, mchele pamoja na sare za shule kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo.