Mufindi FM
Mufindi FM
15 November 2026, 8:27 pm

Dkt. Linda Salekwa awataka viongozi wa Mufindi kuhamasisha wananchi kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote
Na Jackson Machowa
Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Mheshimiwa Dkt. Linda Salekwa, amewataka madiwani na viongozi wengine wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi kuhamasisha wananchi kujiunga na mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ili waweze kupata huduma bora za matibabu kwa gharama nafuu.
Dkt. Salekwa ametoa wito huo wakati akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027, kilichofanyika katika makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, kijijini Itulavanu.

Amesema Serikali ina dhamira ya kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za afya kwa gharama nafuu kupitia mpango huo, hivyo ni wajibu wa kila kiongozi kutumia nafasi yake kuelimisha na kuhamasisha jamii kujiunga na bima hiyo.
Aidha, Dkt. Salekwa amesisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri ili kuiwezesha kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kuboresha huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Mheshimiwa Castory Masangula, amesema halmashauri hiyo imepokea maelekezo yaliyotolewa na ipo tayari kushirikiana na Serikali katika kuyatekeleza kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi kupitia utoaji wa huduma bora.
