Mufindi FM

DC Salekwa: NGO’s zilenge miradi yenye tija kwa wananchi

24 August 2026, 12:10 pm

Mkuu wa wilaya ya Mufindi Mhe. Dkt. Linda Salekwa akizungumza na washiriki katika jukwaa la mwaka la mashirika yasiyo ya kiserikali (NACONGO) lililofanyika ukumbi wa Mbalamaziwa wilayani humo. Picha na Hafidh Ally.

Nitoe rai kwenu naomba tunapoandika maandiko ya kuomba fedha kwa wafadhili, tujitahidi kuangalia hasa kwenye maeneo yenye uhitaji mkubwa ili kuepusha mrundikano wa miradi inayofanana kwenye eneo moja ikiwa kuna sehemu nyingine hakuna kabisa miradi kama hiyo”

Na Marko Msafiri

Mashirika yasiyo ya kiserikali (NACONGO) yamesisitizwa kufanya kazi kwa ukaribu na idara mbalimbali za serikali, lengo ikiwa ni kuepusha mrundikano wa miradi inayofanana katika eneo moja, huku maeneo mengine kukiwa kuna uhitaji mkubwa wa miradi kama hiyo na kwamba wafanye ile inayogusa maisha ya wananchi walio wengi.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya ya Mufindi Mhe. Dkt. Linda Salekwa wakati wa mkutano wa mwaka wa mashirika hayo yasiyo ya kiserikali wilaya ya Mufindi, uliofanyika katika ukumbi wa sambala, uliopo kijiji cha mbalamaziwa, wenye kaulimbiu isemayo “Fikra mpya kuhusu uendelevu na mashirika yasiyo ya kiserikali ubunifu, ubia na upatikanaji wa rasilimali fedha kupitia vyanzo vya ndani”.

Sauti Dkt. Linda Salekwa msisitizo

Vilevile, Dkt. Salekwa ameongeza kwa kuyataka kuwa makini wakati wa utekelezaji wa afua mbalimbali za kusaidia jamii, akisema kuwa kila mradi unapaswa kuchambuliwa kwa kina ili kuhakikisha unaleta maendeleo badala ya kuongeza changamoto au kubomoa kilichojengwa katika jamii.

Sauti Dkt. Linda

Pichani ni Mkuu wa wilaya ya Mufindi Mhe. Dkt. Linda Salekwa (Mgeni rasmi) akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali wa mashirika hayo pamoja na viongozi kutoka serikali ya wilaya ya hiyo. Picha na Hafidh Ally.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mashirika hayo wilaya ya Mufindi, ndg. Fidelis Filipatali ameeleza kuwa lengo la mkutano huo ni kushauriana na kujadiliana pamoja na kuieleza serikali kuhusu namna mashirika hayo yanavyotekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo katika wilayani hapo, sambamba na namna wanavyoweza kujitegemea pasipo kutegemea wafadhili.

Sauti Mwenyekiti NACONGO Mufindi

Mwenyekiti wa mashirika yasiyo ya kiserikali (NACONGO) wilaya ya Mufindi Ndg Fidelis Filipatali akizungumza katika mkutano huo ulifanyika wilayani humo. Picha na Hafidh Ally.

Naye Mratibu wa miradi ya shirika la World Vision Mufindi ya Mufindi Ndg. Zakaria Shibukulu ameongeza kuwa, wamekuwa wakihakikisha miradi mbalimbali inayotekelezwa na shirika hilo inalinda na kuimarisha maadili ya jamii, badala ya kubomoa.

Mratibu wa miradi ya shirika la World Vision wilaya ya Mufindi ndg. Zakaria Shibukulu akizungumza na washiriki katika mkutano huo. Picha na Hafidh Ally.

Akisoma taarifa ya mashirika hayo, Mhe. Marko Shayo ambaye ni katibu wa mashirika hayo wilaya ya Mufindi, amesema katika wilaya hiyo wana mashirika 68, ambapo kwa mwaka wa fedha wa 2025/2026 wametumia zaidi ya Bil 15 katika utekelezaji wa afua mbalimbali wilayani hapo ikiwemo katika Elimu, Afya, Maji, Mazingira, kusaidia watoto, kilimo na kadhalika.