Mufindi FM

Mafunzo ya usawa wa kijinsia katika kilimo yaanza Mafinga

1 October 2026, 2:22 pm

Mkufunzi wa mtandao wa jinsia Tanzania TGNP ndugu Deo Temba {Picha na Christogon Ngoloki}

Jamii imetakiwa kuzingatia ushirikishwaji wa wanawake, vijana wa kike na watu wenye ulemavu katika mnyororo wa thamani wa shughuli za kilimo.

Na Jackson Machowa

Mafunzo ya siku tatu yanayolenga kuwajengea uwezo watoa huduma za maendeleo ya biashara za kilimo (ABD Service Providers) na wadhibiti wa masoko kuhusu usawa wa kijinsia, haki za wanawake na makundi yaliyo pembezoni katika minyororo ya thamani ya kilimo, yameanza rasmi leo mjini Mafinga, Wilaya ya Mufindi.

Mafunzo hayo yanaendeshwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, yakilenga kuongeza uelewa kuhusu nafasi ya wanawake na makundi yaliyo pembezoni katika sekta ya kilimo na namna ya kuwawezesha kupata fursa sawa za kiuchumi.

Washiriki wa mafunzo ya usawa wa kijinsia katika kilimo wakipata elimu

Muwezeshaji kutoka TGNP, Bw. Deogratius Temba, amesema washiriki kutoka sekta binafsi, wauzaji wa pembejeo, taasisi za fedha, wafanyabiashara, serikali za mitaa na Asasi za Kiraia wamekusanywa pamoja ili kujenga uelewa na ushirikiano katika kuimarisha ushiriki wa wanawake kwenye minyororo ya thamani ya kilimo.Mafunzo hayo yanajadili masuala mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, matumizi endelevu ya rasilimali asilia, uhifadhi wa mazingira na nafasi ya wadau katika kuimarisha minyororo ya thamani ya kilimo.

Picha Baadhi ya washiriki wa semina ya mtandao wa jinsia Tanzania TGNP{Picha na Christogon Ngoloki}