Mufindi FM
Mufindi FM
17 November 2026, 11:14 am

TGNP yawawezesha wanawake kupitia mafunzo ya uongozi na jinsia yaliyofanyika Mafinga, yakilenga kuimarisha kujiamini na ushiriki wao katika maamuzi na maendeleo ya jamii.
Na Christogon Ngoloki
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) umetoa mafunzo ya uongozi na jinsia kwa wanawake yaliyofanyika mjini Mafinga, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa, kwa lengo la kuwajengea uwezo wanawake katika masuala ya uongozi na kuongeza ushiriki wao katika nafasi za maamuzi.
Mafunzo hayo ya siku mbili yamewakutanisha wanawake kutoka Wilaya za Kilolo na Mufindi mkoani Iringa, Mbarali mkoani Mbeya pamoja na Wanging’ombe mkoani Njombe.
Akizungumza na Radio Mufindi FM, mwezeshaji wa masuala ya jinsia kutoka TGNP, Deogratius Temba, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mwendelezo wa utekelezaji wa mradi wa Ustahimilivu Wake, Dunia Yetu, unaolenga kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia ushirikishwaji na usawa wa kijinsia katika jamii…….

Temba ameongeza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuongeza uelewa na kuimarisha uwezo wa wanawake katika masuala ya uongozi na jinsia, kuwajengea kujiamini pamoja na kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika nafasi za uongozi na maamuzi kwa ajili ya maendeleo ya jamii.
Kwa upande wao, baadhi ya wanawake walioshiriki katika mafunzo hayo, akiwemo Prisca Mgumba na Jeni Katei, wamesema mafunzo hayo yamewaongezea nguvu, ujasiri na kujiamini katika kuonesha mchango wa wanawake kwa maendeleo ya nchi.
Mradi wa Ustahimilivu Wake, Dunia Yetu, unaofadhiliwa na Shirika la CARE Tanzania na kutekelezwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), unalenga kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika nyanja za kiuchumi, uongozi na kijamii.
