Mufindi FM

ForLand yakutanisha wadau kujadili mazao ya misitu Iringa

12 October 2026, 11:16 am

Wadau wa sekta ya misitu na baadhi ya viongozi wa serikali ngazi ya halmashauri na mkoa wakiwa katika mjadala wa wazi wa kujadili ubora wa mazao ya misitu. Picha na Kelvin Ayubu

Mjadala huo ni miongoni mwa jitihada zinazolenga kuondoa changamoto ya uwepo wa bidhaa za mazao ya misitu yakiwemo magogo yasiyo na ubora sokoni.

Na Jackson Machowa.

Serikali na wadau wa sekta ya misitu mkoani Iringa wamekutana kujadili maendeleo ya sekta hiyo, kwa lengo la kuboresha ubora wa mazao ya misitu na kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi, mkoa na Taifa kwa ujumla.

Mkutano huo umefanyika mjini Iringa kupitia mjadala maalumu wa Talk Show ulioandaliwa na Mradi wa Forland, ukiwa na lengo la kujadili ubora wa mazao ya misitu yanayouzwa sokoni na changamoto zinazokabili mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.

Katika mjadala huo, washiriki, akiwemo Bwana Castory Timbula kutoka taasisi ya TTGAU, wamependekeza kufanyika kwa maboresho pamoja na kuimarishwa kwa usimamizi wa Mwongozo wa Kiufundi wa Sekta ya Misitu wa mwaka 2021, ili kuhakikisha unasimamia ipasavyo mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu nchini.

Sauti ya Castory Timbula kutoka taasisi ya TTGAU akichangia katika mjadala

Kwa upande wake, Mshauri wa Maliasili Mkoa wa Iringa, Dkt. Bahati Goliama, amesema Serikali inaendelea na mchakato wa kuboresha mwongozo huo ili uendane na mahitaji ya sasa na kusaidia ukuaji endelevu wa sekta ya misitu…Wadau Misitu 02..

Sauti Dkt Bahati Goliama mshauri wa maliasili mkoa wa Iringa

Akizungumza na vyombo vya habari, Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa Forland, Emma Nzunda, amesema kuwa licha ya Serikali kuweka viwango vya ubora wa mazao ya misitu, bado kumekuwa na changamoto ya uzingatiaji wa viwango hivyo.

Sauti ya mratibu wa kitaifa wa mradi wa Forland Emma Nzunda

Mjadala huo umefanyika wakati sekta ya misitu ikiendelea kukabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa magogo yenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko, hali inayosisitiza umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa viwango vya ubora na kuboresha mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu nchini.