Mufindi FM

Wananchi Mafinga wakerwa wahudumu hospitalini kuchati badala ya kuwahudumia

24 August 2026, 11:23 am

Wananchi katika kata ya Boma wakimsikiliza Mbunge wa jimbo la Mafinga Mjini Mhe Dickson Nathan Lutevele Villa katika ziara yake ya kikazi ya mtaa kwa mtaa aliyoifanya. Picha na Marko Msafiri.

Wahudumu wa afya katika hospitali yetu wanachati sana Mhe, wanaongea na simu sana kuliko kuhudumia kutuhudumia”

Na Marko Msafiri

Wananchi wa Jimbo la Mafinga Mjini wameeleza kutoridhishwa na utoaji wa huduma katika hospitali ya mji huo, wakidai kuwa baadhi ya wataalamu wa afya hawatoi huduma kwa muktadha unaozingatia mahitaji wa hisia za wagonjwa.

Malalamiko hayo yametolewa wakati wa ziara ya kikazi ya Mbunge wa Jimbo hilo, Mhe. Dickson Lutevele katika mitaa ya Mali ngumu, Mkombwe na Ivambinungu iliyopo katika kata ya Boma ambapo amesikiliza kero mbalimbali zinazowakabili wananchi mbalimbali.

Wananchi hao, wamesema kuna wakati mwingine wanapowapeleka wagonjwa hospitalini hapo, wamekuwa wakikumbana na baadhi ya watumishi ambao badala ya kuwahudumia kwa wakati, huonekana kujishughulisha na simu za mkononi, jambo wanalodai kuwa, linawafanya wajiskie kupuuzwa, sambamba na matumizi ya lugha isiyokuwa rafiki.

Sauti Wananchi

Wananchi wa kata ya Boma wakicheza na Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini Mhe Dickson Nathan Lutevele Villa wakati ya ziara yake katani hapo. Picha na Marko Msafiri.

Akijibu kuhusu kero hizo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo ya Mji Mafinga Dkt. Victor Msafiri amesema atawakumbusha watumishi wa hospitali hiyo kuzingatia taratibu na maadili ya kiutumishi, huku akiwasisitiza wananchi kutokuwa na hofu ya kutoa taarifa pale wanapobaini mtumishi anayekiuka taratibu za kazi au lugha isiyofaa.

Sauti Mganga Mafawidhi Dkt. Msafiri

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, Mhe. Dickson Lutevele Villa amemtaka Mganga huyo Mfawidhi kuhakikisha watumishi wanaelewa mazingira ya kijamii na kiutamaduni wa wananchi wanaowahudumia, kwani kupuuzwa kwao kunaweza kuongeza msongo na kukatisha tama kwa watu wanaokuwa tayari wanapitia changamoto.

Sauti Mbunge Mhe. Dickson Villa

Mbunge wa jimbo la Mafinga Mjini Mhe Dickson Nathan Lutevele Villa akizungumza na wananchi katika kata ya Boma wakati wa ziara yake inayoendelea jimboni humo. Picha na Marko Msafiri.