Mufindi FM
Mufindi FM
26 October 2026, 8:21 pm

KKKT Dayosisi ya Mufindi inatarajia kuchangisha shilingi milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa uzio katika kituo cha Mafinga Child Care Centre, ili kuboresha usalama wa watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu
Na Jackson Machowa
Jamii imetakiwa kushiriki katika kuhakikisha watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu wanapata malezi bora na kukulia katika mazingira salama na rafiki yatakayowawezesha kutimiza ndoto zao kama ilivyo kwa watoto wengine.
Wito huo umetolewa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mufindi mkoani Iringa, ambalo linatarajia kufanya harambee ya kuchangisha shilingi milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa uzio katika kituo cha kulelea watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu cha Mafinga Child Care Centre, kilichopo eneo la Luganga, mjini Mafinga.
Akizungumza na waandishi wa habari Askofu wa kanisa hilo Mch.Dkt Anthony Kipandule amesema kituo cha Mafinga Chirld Care Centre kimeanzishwa mwaka 1972 na kwa miaka mingi kimekuwa kimbilio na msaada kwa watoto yatima na wale wanaotoka katika mazingira magumu jambo linaloisukuma kanisa kuomba nguvu ya wadau ili kuboresha mazingira ya kituo hicho.
Askofu Kipandule ameongeza kuwa kituo hicho kimekuwa kikipokea na kulea watoto bila ubaguzi wa aina yoyote, hivyo kutoa fursa kwa watu kutoka katika dini na madhehebu mbalimbali kushiriki katika harambee hiyo.
Harambee hiyo inatarajiwa kufanyika Oktoba 31, 2026, kituoni Mafinga Child Care Centre, eneo la Luganga, mjini Mafinga kwa kuwakutanisha waumini wa dini na madhehebu mbalimbali, wadau wa maendeleo pamoja na wananchi, kwa lengo la kuunga mkono juhudi za kuhakikisha watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu wanapata malezi bora na kukulia katika mazingira salama.