Mufindi FM
Mufindi FM
9 October 2026, 9:20 pm

Mashirika yasiyo ya kiserikali mkoa wa Iringa yametakiwa kuanza kujitegemea kiuendeshaji badala ya kutegemea ufadhili pekee ili yaweze kuwa endelevu na kusaidia utatuzi wa changamoto zinazoikabili jamii
Na Jumanne Bulali
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) mkoani Iringa yamefanya kongamano la pamoja katika Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, kwa lengo la kutambulisha shughuli, miradi na huduma zinazotolewa kwa jamii, pamoja na kuweka mikakati ya ushirikiano katika kuleta maendeleo ya mkoa huo.
Akizungumza katika kongamano hilo, Mwenyekiti wa mashirika hayo, Fidelisi Filipatali, amesema wamejipanga kushirikiana kwa pamoja katika kutekeleza shughuli zao ili kuongeza ufanisi na kuchangia maendeleo ya wananchi wa mkoa wa Iringa.
Aidha, Filipatali amesisitiza kuwa mashirika hayo hayatasita kutoa taarifa kwa mamlaka husika endapo kutakuwa na shirika lolote litakalokiuka taratibu, ikiwemo ubadhirifu wa fedha, akitaja Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) miongoni mwa taasisi zinazoweza kupokea taarifa hizo.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa mashirika hayo mkoani Iringa, Marco Shayo, ameishukuru Serikali kwa ushirikiano inaoutoa kwa NGOs, akieleza kuwa kongamano hilo limekuwa fursa muhimu ya kujifunza na kupata elimu kutoka kwa taasisi mbalimbali za Serikali.
Miongoni mwa taasisi zilizoshiriki kutoa elimu katika kongamano hilo ni TAKUKURU, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Idara ya Uhamiaji na Maendeleo ya Jamii, ambazo zimechangia kuwajengea washiriki uelewa utakaosaidia kuboresha utekelezaji wa shughuli na miradi yao kwa manufaa ya jamii.