Polisi Zanzibar kufanya kazi na kamati ya maadili
26 November 2024, 7:17 pm
Na Omary Hassan.
Kamishna wa Polisi Zanzibar Cp. Hamad Khamis Hamad amesema kuanzishwa kwa kamati ya Maadili na Elimu ya Afya Zanzibar kutasaidia Jeshi la Polisi katika kutoa elimu kwa wananchi katika kukabiliana na uhalifu na kuporomoka kwa maadili ya jamii.
Akizungumza na Kamati hiyo iliyofika Makao Makuu ya Polisi Zanzibar kwa lengo la kujitambulisha, Cp. Hamad amesema Jeshi la Polisi litashirikiana na kamati hiyo katika kufanikisha majukumu ya Kamati ya Maadili na Elimu ya Afya.
Nae katibu wa Kamati ya Maadili na Elimu ya afya Zanzibar Hamad Bakar Magarawa amesema lengo la Kamati hiyo kufika makao Makuu ya Polisi Zanzibar ni kutafuta ushirikiano na Jeshi la Polisi na kufanyakazi kwa pamoja katika kutoa elimu kwa jamii.
Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya Maadili na Elimu ya Afya Biubwa Ramadhan Said ameiomba jamii kutoa ushirikiano kwa Kamati hiyo wakati wa utoaji wa elimu ya maadili na Afya.