Zenj FM

DCEA yataifisha zaidi ya Tsh. 900m Zanzibar

11 November 2024, 3:09 pm

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya Zanzibar (DCEA) Kanal Burhan Zubeir Nassor akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari huko Ofisini kwake Migombani Wilaya ya Mjini.

Zaidi ya shilingi milioni mia tisa zimetaifishwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya Zanzibar (DCEA) na kuwa mali ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutokana na kupatikana kwa njia ya haramu.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari ofisini kwake Migombani Wilaya ya Mjini Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo, Kanal Burhan Zubeir Nassor amesema zoezi hilo limefanyika kwa mujibu wa sheria namba 8 ya mwaka 2021 ya Mamlaka ya kuthibiti na kupambana na Dawa ya kulevya Zanzibar.

Amesema Mamlaka imetaifisha Kiwanja kilichopo Matemwe na Honda ya aina ya Click, vikiwa na thamani ya Sh. Milioni 422,126, Saleh Khamis Basmani Mkaazi wa Chukwani Wilaya ya Magharibi B na Mke wake Dawari Abas Fakih na kusema Mamlaka inaendelea kuchunguza mali nyengine zilizomo ndani na nje ya Nchi.

Aidha amemtaja Mtuhumiwa mwengine kuwa ni Mohamed Abdalla Juma Mkaazi wa Michenzani Wilaya ya Mjini ambae ni Mtumishi wa Serikali katika Kada ya Sheria ambapo ametaifishwa Kiwanja kilichopo Bweleo Wilaya ya Magharibi B, chenye thamani ya Sh. Milioni 35 baada ya kubainika anashirikiana na Saleh Khamis Basmani katika utakatishaji wa fedha na kuingiza Simu zinazotumika kufanya uhalifu kutoka Nchini Afghanistan.

Hata hivyo amesema Mamlaka imetaifisha Gari aina ya Toyota na Nyumba zilizopo Paje Wilaya ya Kusini, zinazomilikiwa na Andrea Scoph Fres, Raia wa Ujerumani, zenye thamani ya Sh. Milioni 518,926 mara baada ya kukamatwa na Mashine ya kisasa ya kuoteshea Bangi, Polo moja la Bangi pamoja na Shamba la Bangi huko Paje Mkoa wa Kusini Unguja.

Mbali na hayo Kanal Burhan amesema Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya kuthibiti na kupambana na Dawa za kulevya inaendelea kuwatafuta wanaojishughulisha na Dawa hizo ili kunusuru Vijana na utumiaji wa Dawa hizo.

Sauti ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na Dawa za kulevya Zanzibar (DCEA) Kanal Burhan Zubeir Nassor.