Takwimu za matukio ya ukatili wa kijinsia zinatisha Zanzibar
25 November 2024, 3:45 pm
Na Omary Hassan.
Jeshi la Polisi Zanzibar limesema linasimama mstari wa mbele katika kuhakikisha kesi za ukatili wa kijinsia zinashughulikiwa kwa haraka na haki inapatikana kwa wahanga.
Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Hamad Khamis Hamad ameyasema hayo wakati akitoa tamko la Jeshi la Polisi Zanzibar katika kuadhimisha Siku 16 za Kupinga Ukatili Dhidi ya Wanawake na Wasichana.
Kamishna Hamad amesema maadhimisho hayo ni muhimu kwa kuwa hufanya tafakari kwa kina madhara ya ukatili wa kijinsia katika jamii na kuchukua hatua madhubuti za kulinda haki za wanawake na wasichana, ambao ni nguzo muhimu za maendeleo ya taifa.
Ametoa rai kwa jamii kushirikiana kwa karibu na vyombo vya sheria kwa kutoa taarifa kuhusu vitendo vya ukatili vinavyofanyika majumbani, mashuleni, kazini, na katika maeneo ya umma. Amesema Kukaa kimya ni kushiriki katika kuendeleza ukatili.
Aidha amesema Kwa mujibu wa takwimu, matukio ya ukatili wa kijinsia bado yanaripotiwa kwa kiwango cha kutisha. Hali hii inahitaji juhudi za pamoja kati ya serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, asasi za kiraia, viongozi wa dini na jamii kwa ujumla ili kuelimisha watu kuhusu athari za ukatili wa kijinsia na kukuza utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu.
Kaulimbiu ya mwaka ya mwaka huu inakumbusha dhamira ya pamoja ya kuimarisha juhudi za kuzuia ukatili wa kijinsia na kuhakikisha usawa wa kijinsia kwa kila mmoja.