Radio Fadhila
Radio Fadhila
26 November 2026, 15:28 pm

uhamiaji masasi watoa elimu kwa jamii kupitia kampeni ya kitaifa ya mjue jirani yako, kubaini wahamiaji wanaoishi nchini kinyume cha sheria.
Na Godbless Lucius
Idara ya Uhamiaji Wilaya ya Masasi imetoa elimu kwa jamii kuhusu kampeni ya kitaifa ya Mjue Jirani Yako, inayolenga kuwasaidia wananchi kuwafahamu majirani zao, wanakotoka na shughuli wanazofanya, pamoja na kubaini wahamiaji wanaoishi nchini kinyume na sheria na taratibu za uhamiaji.
Akielezea utekelezaji wa kampeni hiyo, Mrakibu Msaidizi wa Uhamiaji Wilaya ya Masasi, Josefu Mabula, amesema kampeni hiyo ni ya kitaifa inayoratibiwa na Idara ya Uhamiaji, ambapo katika Wilaya ya Masasi wanatekeleza kwa kutoa elimu kwa jamii ili kuongeza uelewa na ushiriki wa wananchi katika kutambua wahamiaji haramu.
Ameeleza kuwa wahamiaji haramu wamegawanyika katika makundi mawili, ambapo kundi la kwanza ni wale wanaoingia nchini kupitia njia zisizo rasmi bila kufuata taratibu za uhamiaji, huku kundi la pili likiwa ni wale wanaoingia nchini kupitia njia rasmi lakini kuendelea kuishi nchini baada ya muda wa vibali vyao vya ukaazi kuisha. Aidha, amebainisha kuwa katika ukanda wa Kusini kuna njia tatu rasmi za kuingia nchini ambazo ni Mtambaswala, Mkunya na Kirambo mkoani Mtwara.