Radio Fadhila

Makala ya Fahari yetu :Tanzania yazidi kuboresha miondombinu ya Reli

31 October 2026, 11:35 am

Karibu kusikiliza makala inayoangazia uboreshwaji katika sekta ya usafiri wa reli kupitia miradi mbalimbali inayolenga kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo pamoja na kukuza uchumi. Miongoni mwa miradi hiyo ni maandalizi ya ujenzi wa reli ya kisasa ya Mtwara–Songea–Mbamba Bay itakayounganisha maeneo ya madini na Bandari ya Mtwara, ununuzi wa mabehewa 100 ya mizigo kutoka Uturuki, pamoja na mpango wa kuanzisha treni ya njia moja (Monorail) jijini Dar es Salaam.

Makala ya Fahari yetu tuungane na muandaaji Edwin Mpokasye ambaye kwa wiki hii ameangazia Tanzania inaendelea kupiga hatua katika kuboresha miundombinu ya usafiri wa reli, kupitia miradi mbalimbali inayolenga kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa abiria na mizigo, kuimarisha biashara na kuchochea maendeleo ya uchumi.

Miongoni mwa hatua hizo ni kusainiwa kwa hati ya makubaliano kati ya Shirika la Reli Tanzania, TRC, na kampuni ya Arab Contractors ya Misri, kwa ajili ya kuandaa mradi wa reli ya kisasa ya Mtwara–Songea–Mbamba Bay, utakaounganisha pia maeneo ya uchimbaji madini ya Liganga na Mchuchuma.

Mradi huo unakadiriwa kuwa na urefu wa jumla wa kilomita elfu moja, ukiwa na lengo la kuunganisha Bandari ya Mtwara katika Bahari ya Hindi na maeneo mbalimbali ya uzalishaji na biashara kusini mwa Tanzania.
Reli hiyo inatarajiwa kurahisisha usafirishaji wa madini ya chuma, makaa ya mawe, mazao ya kilimo na bidhaa za viwandani, pamoja na kufungua fursa mpya za biashara na nchi jirani zikiwemo Malawi, Msumbiji na Zambia.