Radio Fadhila

Bi Harusi Afariki Dunia siku ya Ndoa yake

21 September 2026, 13:58 pm

Ni simanzi katika kijiji cha Nambaya ambapo Bi Flaviana Hokororo, 37, amefariki dunia siku ya ndoa yake huku chanzo rasmi cha kifo chake kikiwa bado hakijajulikana. Mashuhuda wanasema hali yake ilibadilika ghafla wakati maandalizi ya ndoa yakiendelea

Na Godbless Lucius

Bi Harusi Flaviana Hokororo, mwenye umri wa miaka 37 na mkazi wa Kijiji cha Nambaya Masasi, amefariki dunia siku ambayo alitarajiwa kufunga ndoa. Kwa mujibu wa taarifa marehemu alikuwa ni mjamzito wa mwezi mmoja. Hata hivyo, chanzo rasmi cha kifo chake bado hakijawekwa wazi

Mume wa marehemu, Patric Almasi, amesema “Hakuwa na nguvu kabisa. Nikamwambia mke wangu, mimi nakupenda na nina nia ya dhati kabisa ya kufunga ndoa na wewe. Kwa kuwa nina nia ya dhati kabisa ya kukuoa, naomba tufunge ndoa hapa hapa tulipokuwepo,” amesema Patric.

Sauti ya Mume wa marehemu, Patric Almasi

Kwa upande wake, Sister Devota Maluma, muuguzi wa Zahanati ya Nambaya, amesema hali ya marehemu ilibadilika ghafla na damu ilishuka, huku wahudumu wa afya wakijitahidi kuokoa maisha yake.

“Inaonekana alikuwa na ujauzito wa mwezi mmoja, lakini naona mara tu damu imeshuka. Binafsi, mgonjwa tulimpambania. Lengo lilikuwa awe katika hali nzuri,” amesema Sister Devota.

Sauti ya Sister Devota Maluma

Naye Padre Ignas Mlelwa, aliyekuwa akiongoza ibada ya ndoa , amesema “Kabla ya ndoa yake aliungama dhambi zake vizuri. Tunajiuliza maswali huko mtaani, tunamtafuta mchawi, lakini hakuna mchawi. Mungu ndiye mwenye mamlaka,”.

Mashuhuda wa tukio hilo wameeleza kuwa hali ilibadilika ghafla wakati maandalizi ya ndoa yakiendelea. Kwa mujibu wa mmoja wa majirani, marehemu alikuwa ameketi, lakini baadaye alianguka ghafla na hali yake ikawa mbaya.