Radio Fadhila

Masasi yasisitiza lishe bora kwa maendeleo ya elimu

17 September 2026, 21:22 pm

Halmashauri ya Wilaya ya Masasi imeendelea kuimarisha afua za lishe kwa jamii kwa kukabidhi Watendaji wa Kata vitabu vyenye matokeo ya utafiti wa hali ya lishe katika kata mbalimbali. Vitabu hivyo vimekabidhiwa Septemba 17, 2026, na Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Mhe. Rachel Kassanda, wakati wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwa robo ya nne ya mwaka wa fedha 2025/2026.

Na Godbless Lucius

Halmashauri ya Wilaya ya Masasi imeendelea kuimarisha utekelezaji wa afua za lishe kwa jamii, baada ya Watendaji wa Kata kukabidhiwa vitabu vyenye matokeo ya utafiti wa hali ya lishe katika kata mbalimbali za Halmashauri hiyo.

Vitabu hivyo vimekabidhiwa leo, Septemba 17, 2026, na Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Mhe. Rachel Kassanda, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Lishe ngazi ya jamii, wakati wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa Mkataba wa Lishe ngazi ya jamii kwa robo ya nne, Aprili hadi Juni 2026, kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Kassanda amewataka Watendaji wa Kata kutumia taarifa za utafiti huo katika kuimarisha uhamasishaji na utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa lishe bora, hususan kwa watoto na wanafunzi.

Amesisitiza kuwa lishe bora ni msingi muhimu katika ukuaji na maendeleo ya mtoto, afya njema pamoja na kuongeza uwezo wa mwanafunzi kujifunza na kufanya vizuri shuleni.

Aidha, Mhe. Kassanda amepongeza jitihada zinazofanywa na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji pamoja na Maafisa Lishe katika kuimarisha elimu ya lishe shuleni na kwenye jamii, ikiwemo uhamasishaji kuhusu urutubishaji wa chakula na udhibiti wa udumavu.