Radio Fadhila

Onyo la Mtwara, Lindi na Ruvuma kwa wafugaji wasio na vibali

25 October 2026, 15:48 pm

Kamati za Usalama za Mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma zasimamia juhudi za kudhibiti migogoro ya wakulima na wafugaji kwa kusisitiza uzingatiaji wa sheria, matumizi sahihi ya vitalu na ushirikiano wa wananchi.

Na Godbless Lucius

Kamati za Usalama za Mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma zimewaonya wafugaji wanaohamisha mifugo bila vibali na kusisitiza kuwa hatua zitachukuliwa dhidi ya watakaokiuka sheria na taratibu za ufugaji.

Onyo hilo limetolewa Oktoba 24, 2026, katika kikao cha pamoja cha Wakuu wa Mikoa hiyo na Kamati zao za Usalama kilichofanyika Wilaya ya Nanyumbu, mkoani Mtwara, kwa lengo la kujadili changamoto za usalama na kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana nazo.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Adam Malima, amesema viongozi hao wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika kukabiliana na uhalifu, ikiwemo kuwafuatilia wanaokimbilia wilaya au mikoa jirani baada ya kutenda makosa.

Mhe. Adam Malima

Mhe. Malima pia amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika kudumisha usalama kwa kutoa taarifa na kushirikiana na vyombo husika katika kuwabaini wahalifu.

Kuhusu uhamishaji wa mifugo, amesema kumekuwa na ongezeko la mifugo inayohama kutoka eneo moja kwenda jingine bila vibali, huku baadhi ya wafugaji wakishindwa kutumia vitalu walivyotengewa na badala yake kuiacha mifugo yao kuingia na kuharibu mashamba ya wakulima.

“Tanzania ni ya wote, lakini kila mtu anapaswa kuishi kwa kufuata misingi ya sheria na taratibu. Wafugaji tumewapa vitalu, lakini hamvitumii; mnaacha mifugo yenu inaenda kuharibu mashamba ya watu. Tutachukua hatua,” amesema Mhe. Malima.