Karagwe FM

Uwepo wa Paka Dhahabu katika hifadhi asilia ya msitu wa Minziro, Tanzania

4 December 2022, 3:03 pm

Msitu wa Minziro ni msitu mnene wenye bionuai ya kepee unaopatikana Tanzania. Msitu huu unaomilikiwa na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) upo katika Wilaya ya Missenyi Mkoani Kagera. Makao makuu ya Ofisi ya Hifadhi ya Asilia ya Minziro yapo Bunazi. Msitu huu kwa upande wa kaskazini unapakana na nchi ya Uganda ambapo kuna hifadhi nyingine iitwayo Sango Bay. Kwa upande wa Kusini na Mashariki, msitu huu umepakana na Mto Kagera na kwa upande wa Magharibi umepakana na Barabara kuu iendayo nchini Uganda. Vile vile una ukubwa wa eneo la kilometa za mraba 257 na uzio wa mpaka wenye urefu wa kilometa 80.Licha ya kuwa na viumbe vya kipekee na adimu kupatikana katika misitu mingine hapa Tanzania, pia una umuhimu mkubwa sana katika bonde la Mto Kagera ambapo takribani kaya 8500 zenye watu zaidi ya elfu 40 kutoka katika vijiji nane wanaishi jirani na Msitu huu.

Ugunduzi wa Paka dhahabu Tanzania

Picha ya paka dhahabu

Mnamo mwaka 2018, watafiti kutoka Chuo cha Usimamizi waWanyamapori na kituo cha utafiti cha Udzungwa, Tanzania kwa kushirikiana na watafiti kutoka nchini Italia walifika kwenye hifadhi hii ili kuidadi aina ya viumbe na bionuai iliyopo kwenye hifadhi hii. Miongoni mwa gunduzi muhimu ni uwepo wa Paka dhahabu ambaye kwa lugha ya kiingereza anaitwa “African Golden Cat“. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, paka huyu ambaye anapatikana tu katika bara la Afrika tayari alishagunduliwa siku nyingi kuwepo katika mataifa mengine ya Afrika hususani yale ambayo misitu minene ya Guinea-Congo imepita kama Cameroon, Africa ya kati, DRC na Gabon. Nchi zingine ambapo huyu paka ameripotiwa kuwepo ni pamo jana Kenya na Uganda.

Sifa za paka huyu

·      Ni mnyama msiri sana na mara nyingi hupendelea kufanya shughuli zake za mawindo usiku;

·      Mara nyingi hupendelea faragha;

·      Chakula chake kikubwa ni wanyama wadogo wadogo kama pimbi, digidigi, funo, ndege na samaki;

·      Ana uwezo wa kuishi hadi miaka 15 katika mazingira yake ya asili na hadi miaka 17 kwenye mazingira ya kufugwa;

· Akiwa mkubwa anafikisha uzito kati ya kilo 5.5 – 16, kima chake ni sentimita 38 – 55 na urefu kutoka mdomoni hadi ncha ya mkia ni sentimita 61 – 101.

Licha ya habari nzuri hii ya uwepo wake, paka huyu, lakini tafiti zionaonyesha paka huyu yupo mbioni kutoweka kutokana na sababu zifuatazo:

·         Uwindaji haramu wa wanyamapori

·         Uchomaji moto wa misitu

·         Kulisha mifugo ndani ya Hifadhi

·         Kukata kuni au magogo ndani ya hifadhi

Nini kifanyike

Chuo cha Usimamizi wa wanyapori Mweka kwa kushirikiana na wakala wa misitu Tanzania, chini ya ufadhili wa mfuko wa Uhifadhi wa taasisi ya Mohamed Bin Zayed, kiliandaa program maalum ya ushirikiswaji wa jamii katika kuandaa mikakati ya kiuhifadhi kukabiliana na changamoto zinazotishia ustawi wa paka dhahabu, misitu ya minziro, Tanzania. Miongoni mwa vitu vilivyotiliwa mkazo ni pamoja na haya:

Wananchi washirikishwe katika miradi endelevu ambayo itapunguza utegemezi wa moja kwa mojawa mazao yatokanayo na msitu ya asili wa Minziro;

·         Wananchi wajiunge kwenye vikundi vidogo vidogo vya ujasiriamali kama ufugaji ili waweze kupata protini kutokana na ufugaji na pia fedha baada ya kuuza mifugo;

·         Mamlaka za uhifadhi hususani TFS iimarishe shughuli za kupambana na ujangili;

·         Wananchi wahamasishwe kutumia majiko banifu; na

·         Wananchi wahamasishwe kutumia mpango mzuri wa matumizi bora ya ardhi ya kijiji (Village Land Use Plan)

Kwa mawasiliano zaidi:

emmanuel.martin2@mwekawildife.ac.tz