Buha FM Radio

Bunge Lachunguza Ubora wa Huduma za Afya Kasulu

9 November 2026, 5:34 pm

Naibu waziri wa afya Dkt Florence Samizi Akikagua maendeleo ya utoaji huduza za afya katika Halmashari ya mji Kasulu. Picha na Paulina Majaliwa

Halmashauri ya Mji Kasulu Mkoani Kigoma imepongezwa kwa kuendelea kupiga hatua katika utoaji wa huduma za afya hasa kwa kupunguza vifo vya mama na mtoto hayo yamebainishwa baada ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya pamoja na Shirika lisilo la kiserikali la Thamini Uhai kufanya ziara ndani ya halmashauri hiyo.

Na; Paulina Majaliwa.

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na masula ya UKIMWI kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la Thamini Uhai imefanya ziara ya mafunzo katika kituo cha afya cha Kiganamo pamoja na Hospitali ya halmashauri ya mji Kasulu (hospitali ya Mlimani) lengo ni kutathmini ubora wa huduma za afya.

Akizungumza katika ziara hiyo Naibu waziri wa afya Dkt Florence Samizi amewaomba watumishi wa afya kujiandaa kupokea wagonjwa wenye bima ya afya kwa wote huku akiwasisitizia kutumia lugha nzuri na ubora wa huduma kwa wagonjwa.

Sauti ya Naibu waziri wa afya Dkt Florence Samizi

Aidha ameipongeza Halmashauri ya mji Kasulu kwa kutumia mapato ya ndani kukarabati miundombinu ya hospitali na vituo vya afya pamoja na kuendeleza kampeni ya Mjamzito na Mtoto Salama kwa lengo la kuwasimamia na kuwaongoza katika kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Sauti ya Naibu waziri wa afya Dkt Florence Samizi
Kamati ya kudumu ya bunge na wadaau wa SHIRIKA LA Thamini Uhai wakiendelea na mafunzo ya Afya. Picha na Paulina Majaliwa.

Kadhalika Dkt Samizi amewahimiza waganga wakuu wote kupitia mwongozo wa wizara ya afya kuhusiana na mwambata wa mama mjamzito na kupitia ramani ya ujenzi wa wodi ya kujifungulia yenye utu heshima na staha ili kupunguza vifo vya mama na mtoto ifikapo 2030.

Sauti ya Naibu waziri wa afya Dkt Florence Samizi

Naye Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya afya na UKIMWI Mhe. Emanuel Nuwas amesema changamoto zote zilizowasilishwa na hospitali zote za mkoa wa Kigoma zitaenda kufanyiwa kazi na kamati husika huku akiwataka wahudumu wa afya kuendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Halmashauri, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Luteni Kanali Joseph Murimi ameishukuru Serikali kupitia Kamati hiyo kwa ziara na maelekezo yaliyotolewa wakiahidi kuyafanyia kazi ili kuboresha huduma za afya.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Thamini Uhai Banzi Msumi akizungumza katika mafunzo hayo. Picha na Paulina Majaliwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Thamini Uhai Banzi Msumi amemshukuru Rais kupitia wizara ya afya na TAMISEMI kwa kuendelea kuunga mkono sera ya usalama wa mama mjamzito na mtoto hali ambayo imepelekea kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Thamini Uhai ni shirika lisilo la kiserikali linalofanya kazi kwa ushirikiano na Serikali kupunguza vifo vya mama Mjamzito na Mtoto, hasa katika maeneo ya vijijini huku likiwa na Mradi wa “Mjamzito na Mtoto Salama” Mradi unaolenga kuimarisha huduma za afya ya uzazi na watoto katika mikoa mbalimbali.