Buha FM Radio

Kasulu DC yajipanga kukabiliana na mvua za El Niño

16 October 2026, 2:15 pm

Mratibu wa Kamati ya Maafa katika halmashauri hiyo, Fadhili Simon Ndunguru. Picha na Alfred Lukonge Afisa Habari Kasulu DC.

Kamati ya Maafa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma imesema imejiandaa kukabiliana na athari za mvua za El Niño, huku wananchi wakitakiwa kuchukua tahadhari na kuepuka maeneo hatarishi.

Na; Paulina Majaliwa

Kamati ya Wataalamu ya Usimamizi wa Maafa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma, imesema imejiandaa kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño kupitia mikakati iliyowekwa na kila kitengo ndani ya kamati hiyo.

Akizungumza na Buha FM Radio kupitia kipindi cha Darasa Nje ya Shule, Mratibu wa Kamati ya Maafa katika halmashauri hiyo, Fadhili Simon Ndunguru, amesema pamoja na mikakati iliyowekwa, wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari kwa kutambua maeneo hatarishi na yale yenye historia ya kujaa maji, kuepuka kutembea au kuogelea kwenye maji yaliyotuama, pamoja na kuhama katika maeneo ya maporomoko ya ardhi.

Sauti ya Fadhili Simon Ndunguru.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TANESCO Wilaya ya Kasulu, Venance Kassian, amesema shirika hilo limejiandaa kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza katika kipindi cha mvua hizo, na amewataka wananchi kuchukua tahadhari kwa kukagua miundombinu ya umeme, kuepuka kuanikia nguo kwenye nyaya za chuma, kutokujiunganishia umeme kiholela na kukaa mbali na miundombinu ya umeme.

Sauti ya Venance Kassian.
Kaimu Meneja wa TANESCO Wilaya ya Kasulu, Venance Kassian. Picha na Raymond Kalalu Afisa Habari Kasulu DC.

Naye Kaimu Meneja wa RUWASA na Fundi Sanifu katika ofisi ya RUWASA Wilaya ya Kasulu, Bi. Ikaanami Mruth, amesema mamlaka hiyo imejiandaa kwa kuunda kamati mbalimbali zitakazoshughulikia kwa haraka hitilafu zinazoweza kujitokeza.

Aidha, amewataka wananchi kuchukua tahadhari kuhusu usalama wa maji kwa kusisitiza matumizi ya maji salama yanayotoka kwenye mabomba yanayosimamiwa na mamlaka husika, huku wakiepuka kutumia maji ya visima ambayo hayajathibitishwa kuwa salama kwa matumizi ya binadamu.

Sauti ya Bi. Ikaanami Mruth.
Kaimu Meneja wa RUWASA na Fundi Sanifu katika ofisi ya RUWASA Wilaya ya Kasulu, Bi. Ikaanami Mruth. Picha na Alfred Lukonge, Afisa Habari Kasulu DC.

Akizungumza kwa niaba ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, S/SGT Africanus Erasmus Mrema, amesema maeneo ya kuwahifadhi wananchi watakaohamishwa kutoka maeneo hatarishi yameandaliwa. Amewataka wananchi wanaoishi katika maeneo hayo kuhama mapema ili kujiepusha na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño.

Sauti S/SGT Africanus Erasmus.
S/SGT Africanus Erasmus Mrema kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu. Picha na Raymond Kalalu Afisa Habari Kasulu DC.

Katika hatua nyingine, wawakilishi wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania (Tanzania Red Cross), msimamizi wa chama hicho Wilaya ya Kasulu, Mateo Baltazar, pamoja na Mwenyekiti wa chama hicho wilayani humo, Wilbrod John, wamewataka viongozi wa mitaa kutoa ushirikiano kwa kamati za maafa ili kuwezesha hatua za haraka kuchukuliwa pale changamoto zinapojitokeza.

“Niwahamasishe matawi yote tuliyokuwa nayo ili yaendelee kutmika kama ilivyokuwa hapo awali” Amesema msimamizi wa Red Cross Mateo Baltazar.

Msimamizi wa chama cha Tanzania Red Cross Wilaya ya Kasulu, Mateo Baltazar. Picha na Alfred Lukonge, Afisa Habari Kasulu DC.

“Tunaomba rai wananchi waliopo katika maeneo hatarishi kuchukua hatua za kujiokoa bila kusubili kuolewa poja na wale ambao hawajafunika visima vya maji wafunike ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza”Amesema Mwenyekiti Wilbrod John.

Mwenyekiti wa chama Msalaba mwekundu wilayani Kasulu Wilbrod John. Picha na Alfred Lukonge, Afisa Habari Kasulu DC.

Kamati hiyo imewataka wananchi kutoa taarifa mapema endapo kutatokea dharura, kwa kupiga simu namba 114 kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, 180 kwa TANESCO, na 0767044255 kwa RUWASA kwa ajili ya kupata msaada wa haraka.