Buha FM Radio
Buha FM Radio
12 December 2025, 7:50 pm

Baadhi ya wananchi mkoani Kigoma wameeleza ugumu wanaopitia katika swala la kutoa taarifa za maswala ya ukatili wa kijinsia wakihofia usalama wao baada ya kutoa taarifa hizo.
Na; Irene Charles
Katibu tawala mkoa wa Kigoma Ndg. Hassan Rugwa amesema viongozi husika wa maswala ya ukatili wanatakiwa kujifunza kupitia viongozi wengine na kushirikisha watu mbalimbali kwenye utatuzi wa kesi za ukatili.
Amesema hayo wakati wa maadhimisho ya kilele cha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia katika Chuo cha Ualimu Kasulu (TTC) amesema kutambua viongozi mbalimbali inasaidia kuongeza ushirikiano wa kupinga matukio ya ukatili katika jamii.
Nao baadhi ya wananchi walioudhuria maadhimisho hayo wamesema wanaogopa kutoa taarifa wakiofia usalama wao na kueleza kuwa hupuuzwa wanapopeleka taarifa kwa viongozi wanaohusika huku wakiomba serikali kuendelea kutoa elimu katika jamii.

Baadhi ya wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo katika maadhimisho ya kilele cha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia mkoani Kigoma. picha na Irene Charles.
Aidhai Afisa maendeleo Mkoa wa Kigoma Msafiri Nzunubi amesema hali ya vitendo vya ukatili katika mkoa huo kwa sasa imepungua kutokana na utafiti wa takwimu za kitaifa ikiwa sasabu kubwa ni wananchi kuendelea kupata elimu ya kutosha.
Katika hatua nyingine Ndg. Msafiri amesema licha ya kupungua kwa vitendo vya ukatili lakini bado vitendo hivyo vipo na kuwaomba wananchi kutoa taarifa na kujitokeza kutoa ushirikiano katika vyombo vya dola kwa lengo la kupunguza matukio hayo.
Mrakibu msaidizi wa jeshi la polisi na mkuu wa dawati la kijinsia na watoto mkoani Kigoma Ndg. Michael Mjema amesema wametoa elimu katika Wilaya na Halmashauri zote zilizopo ndani ya Mkoa huo kwa kuzingatia makundi mbalimbali.
Sanjari na hayo Ndg. Mjema amesema baadhi ya kesi hazifiki mwisho kutokana na wananchi kutofika mahakani, pia ametoa rai kwa jamii kutosuruhisha matukio ya ukatili bali wafike na kutoa ushirikiano katika vyombo husika.

Maadhimisho ya kilele cha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa mwaka 2025, kwa Mkoa wa Kigoma yamefanyika katika Halmashauri ya Mji Kasulu yakiwa yamebebe kaulimbiu ya “Tuungane pamoja katika Kutokomeza Ukatili Mitandaoni”.