Buha FM Radio
Buha FM Radio
27 June 2026, 5:14 pm

Wananchi wilayani Uvinza wawasilisha kero zao kwa Mkuu wa Wilaya Mh. Dinah Mathamani ambapo tayali baadhi ya kero zimetolewa ufafanuzi.
Na; Mwandishi wetu
Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mh. Dinah Mathamani, amefanya ziara katika Kata ya Uvinza kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili wananchi.
Akizungumza na wananchi, Mh. Dinah amesema changamoto ya mabasi kutofika stendi ya mwisho imepatiwa ufumbuzi kufuatia kuanza rasmi kwa shughuli katika Stendi ya Wilaya hiyo.
Aidha Mh. Dinah ameagiza mabasi yote yaliyosajiliwa kutoa huduma hadi Uvinza yafike stendi hiyo kuanzia leo maagizo ameyatoa baada ya kusikiliza kero za wananchi waliolalamika kuhusu changamoto ya usafiri wanapofika standi ya mabasi ya Wilaya.

Katika Hatua nyingine Mh. Dinah amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itaandaa eneo bora kwa ajili ya shughuli za michezo na burudani pamoja na kuwasisitiza maafisa wa Jeshi la Polisi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia haki na sheria ili kuimarisha uhusiano mzuri na wananchi.

Mh. Dinah amehitimisha kwa kuzungumzia mgogoro wa ardhi unaoikabili Kata ya Ruchugi, ambapo ameahidi kuushughulikia kwa kushirikiana na mamlaka husika ili kupata suluhisho la kudumu la mgogoro huo.