Buha FM Radio

Zaidi ya 500 wahudumiwa kibingwa Hospitali ya Rufaa Kabanga

17 April 2026, 5:06 pm

Mganga Mfawidhi wa hospitali ya rufaa Kabanga Dkt. Peter Kitenyi wakati akieleza namna zoezi la kuwahudumia wananchi linavyoendelea. Picha na Sharifat Shinji.

“Lengo la hospitali yetu ni kuwasaidia wagonjwa kwa ukaribu zaidi kama sera ya wizara ya afya inavyotaka hivyo hata sisi tumesogeza huduma hizi za kibingwa ili kurejesha matumaini ya wananchi wa Kasulu na maeneo mengine jirani” Amesema Dkt. Kitenyi.

Na; Sharifat Shinji

Zaidi ya wananchi 500 wa Wilaya ya Kasulu na Mkoa wa Kigoma kwa ujumla wamenufaika na huduma ya Kambi ya madaktari bingwa inayoendelea katika hospitali ya Rufaa Kabanga iliyopo wilayani Kasulu katika Mkoa wa Kigoma.

Hayo yameelezwa na Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Dkt. Peter Kitenyi wakati akieleza jinsi zoezi la utowaji huduma kwa wananchi, ambapo amesema mwitikio wa  wananchi kufika katika hospitali hiyo ni mkubwa huku akitaja zaidi ya wananchi 500 wameshapata huduma ya kuonana na madakitari hao.

Sauti ya Dkt. Kitenyi.

Aidha Dkt. Kitenyi ameeleza huduma mbalimbali zinazotolewa katika kambi hiyo ya madaktari bingwa  ambapo amesema lengo nikuwahudumia wananchi wa Wilaya ya Kasulu kwa ukaribu zaidi huku akitoa pongezi kwa wafanyakazi wote wa hospitali hiyo.

Sauti ya Dkt. Kitenyi.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza kupata huduma za kibingwa katika Hospitali ya Rufaa Kabanga. Picha na Sharifat Shinji.

Kwa upande wake Evarist Mwelongo ambaye amezungumza kwa niaba ya wagonjwa wengine amesifia huduma aliyoipata kutoka kwa madakitari bingwa wa meno huku akiwasisitiza wananchi wengine kutumia furusa ya Kambi hiyo kufanya vipimo vya uchunguzi wa afya zao.

Sauti ya Mwelongo mwananchi aliyepata huduma hospitalini hapo.

Hospitali ya Rufaa Kabanga imekuwa na utaratibu wa kuendesha kambi za madakitari bingwa kila mwezi ikiwa mwezi huu kambi hiyo imeanza April 13 hadi April 17 huku zaidi ya wananchi 500 wakiwa wamefika kupata huduma katika hospitali hiyo.

Daktari wa idara ya Kinywa na Meno akitoa huduma kwa Mgonjwa aliyefika katika Hospitali hiyo kupata huduma. Picha na Shinji.