Buha FM Radio

Operesheni ya Wakimbizi kurudishwa kwao Madiwani waombwa kusimamia

22 April 2026, 12:04 am

Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Mhe. Kanal Isaack Mwakisu akitoa maelekezo kwa Madiwa wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu. Picha na Sharifat Shinji.

“Kigoma ndo Mkoa pekee umebaki na wakimbizi wengi kuliko maeneo yote, Nyarugusu pekee inahudumia zaidi ya wakimbizi 140,000 kwahiyo hakikisheni mnasimamia kikamilifu zoezi la raia hawa wa kigeni wanarudishwa kwao pamoja na kushirikiana kutoa tarifa za raia walioingia kinyume na sheria za nchi.” Amesema Mwakisu.

Na; Sharifat Shinji

Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Mhe. Kanal Isaack Mwakisu ametoa maelekezo kwa Madiwa wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kuhakikisha wanaendelea kusimamia operesheni za kurudishwa kwa wakimbizi na raia wa Burundi waliopo katika kambi za Nduta na Nyarugusu.

Maelekezo hayo ameyatoa leo wakati akiwasilisha ujumbe wa Serikali katika kikao cha robo ya tatu cha baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, ambapo amesema serikali kwa kushirikiana na wasimamizi wa kambi wamekubaliana kurudishwa kwa wakimbizi hao katika nchi zao  jambo ambalo linaendelea katika kambi hizo.

Sauti ya Mkuu wa Wilaya.

Aidha kwa upande wake Diwani wa kata ya Kurugongo Edison Hanyuma amesema swala la ulinzi na usalama wa wananchi si swala la Mkuu wa Wilaya bali ni kila mwananchi ana wajibu wa kutoa ushirikiana kubaini raia wanaoingia nchini bila kufuata sheria na taratibu zilizowekwa.

Sauti ya Diwani Hanyuma.
Baadhi ya Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu wakiwa katika Kikao cha Robo ya tatu cha Baraza la Madiwani. Picha na Sharifat Shinji.

Katika hatua nyingine Diwani wa kata ya Kitanga Eliya Kagoma ameeleza wajibu wao katika kuhakikisha wanadhibiti wahamiaji haramu huku akieleza jinsi ambavyo raia hao wamekuwa wakitumika katika shughuli za uzalishaji hasa kilimo ambapo amesema watatoa elimu kwa wananchi wanaowatumia raia hao wa kigeni.

Sauti ya Diwani Kagoma.

Kwa muujibu wa maelezo ya Mkuu wa Wilaya, amesema Kigoma ni miongoni wa Mikoa inayohudumia wakimbizi wengi zaidi, huku Kambi ya Nyarugusu inahudumia wakimbizi zaidi ya 100,000 jambo ambalo serikali imechukua hatua madhubuti za kuwarejesha kwao kutokana na hali ya utulivu kurejea katika nchi zao hasa nchi ya Burundi.

Diwani wa kata ya Kitanga Eliya Kagoma akisoma tarifa mbele ya Baraza la Madiwani. Picha na Sharifat Shinji.