Buha FM Radio
Buha FM Radio
10 May 2026, 5:16 pm

Jamii yasisitizwa kufanya mazoezi ili kukabiliana na magonjwa yasiyoambukizwa.
Na; Sharifat Shinji
Hospitali ya Rufaa Kabanga imezindua klabu ya mazoezi (Jogging Club) ikiwa ni juhudi za kuunga mkono serikali kupunguza wimbi la magonjwa yasiyoambukizwa ambapo kila Jumamos klabu hiyo itafanya mazoezi kwa kufuata ratiba itakayokuwa inatolewa na uongozi wa klabu hiyo.
Uzinduzi huo umefanyika jana Jumamosi katika uwanja wa mpira wa miguu Miembeni mkabala na Hospitali hiyo, katibu wa hospitali Flora Laurian Ntahondi amesema kuanzishwa kwa klabu hiyo ni kuunga mkono juhudi za serikali za kukabiliana na magonjwa yasiyoambukizwa ikiwemo saratani.

Kwa upande wake Afisa Michezo Halmashauri ya Mji Kasulu Bw. Venatus Edward ambaye alikuwa mgeni rasmi katika zoezi hilo ameipongeza hospitali ya rufaa Kabanga kwa kuunda klabu hiyo na kusema jamii inapaswa kuchukua maamuzi sahihi ya kufanya mazoezi ili kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na mtindo wa maisha.

Zoezi hilo liliambatana na mbio (Jogging) ambazo zilifanyika kwa kuzunguka eneo la hospitali, zikihusisha wafanyakazi wa Kabanga, wananchi pamoja na wanafunzi wa Chuo cha Afya Kabanga huku kauli mbiu ikiwa nia “kimbia pamoja, baki na afya njema, na ufurahie mtindo wa maisha bora”
