Buha FM Radio
Buha FM Radio
28 July 2026, 11:50 am

Kutokana na changamoto ya migogoro ya ndoa na ndoa nyingi kuvunjika,viongozi wa Madhehebu mbaalimbali wilayani Kasulu wameombwa kusimami kwa ukamilifu zoezi la ufungishaji wa ndoa, wakitakiwa kuwa na leseni au bibali vya ufungishaji wa ndoa.
Na; Paulina Majaliwa
Serikali imewataka viongozi wa makanisa wilayani Kasulu mkoani Kigoma kuhakikisha wachungaji wanaofungisha ndoa wanakuwa na vibali au leseni halali na zilizo hai, hatua itakayorahisisha utatuzi wa migogoro ya ndoa pamoja na kulinda uhalali wa ndoa zinazofungwa nchini.
Wito huo umetolewa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kasulu, Bi. Theresia Mtewele, wakati wa hafla ya kumsimika Askofu wa Jimbo la Kigoma kupitia Kanisa la Hope For All Nations (HOFAN), iliyofanyika katika Halmashauri ya Mji Kasulu ambapo amesema ndoa zinazofungishwa na viongozi wenye leseni halali hurahisisha kazi ya Msajili wa Ndoa na vyombo vya serikali kushughulikia migogoro ya kifamilia, hali inayoweza kupunguza ongezeko la watoto wanaoishi mitaani.
Aidha, Bi. Mtewele amewataka viongozi wa dini kushirikiana na waumini pamoja na jamii kuwaandaa vijana kwa misingi bora ya ndoa na maadili, ili kupunguza kasi ya kuvunjika kwa ndoa kunakotokana na sababu zisizo za msingi.
Kwa upande wake, Kiongozi Mkuu na mwanzilishi wa Kanisa la Hope For All Nations (HOFAN), Askofu Dkt. Charles Jangalason, amesema umoja na mshikamano ni msingi muhimu wa maendeleo ya taifa na kuwataka viongozi wa kanisa hilo kuwafundisha waumini misingi ya imani ya kweli ili kuepusha taharuki, migawanyiko na migogoro ndani ya kanisa na katika jamii kwa ujumla.

Naye Askofu mteule wa Jimbo la Kigoma, Askofu Alex Kalalaye, amewashukuru viongozi na waumini wa kanisa hilo kwa kumuamini na kumpa jukumu la kuliongoza jimbo hilo pamoja na kutoa ahidi ya kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Wilaya ya Kasulu katika kudumisha amani, umoja na maendeleo ya jamii.
