Buha FM Radio
Buha FM Radio
29 July 2026, 6:58 pm

Kufuatia kuanza kwa mwaka mpya wa fedha, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu amewataka watumishi na viongozi kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uwajibikaji na ushirikiano ili kuhakikisha vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita vinatekelezwa kwa ufanisi.
Na; Ramadhan Zaidy
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma wametakiwa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uwajibikaji na ushirikiano ili kuhakikisha vipaumbele vya Serikali vinatekelezwa kwa ufanisi na kuwanufaisha wananchi.
Wito huo umetolewa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kasulu, Bi. Theresia Mtewele, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya katika kikao cha robo ya nne cha Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo. Amesema ni muhimu kwa kila diwani kuhakikisha anatoa mrejesho kwa wananchi kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo anayoyawakilisha.

Naye Mbunge wa Jimbo la Kasulu Vijijini, Edibily Kazala, amewashukuru madiwani kwa ushirikiano wanaoendelea kumpa katika kusimamia na kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo ndani ya jimbo hilo.
Kwa upande wao, baadhi ya madiwani wa Halmashauri hiyo wamesema fedha zilizotengwa na Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027 zimeanza kufika katika maeneo yao, hatua ambayo itasaidia kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi.

Akiwasilisha salamu za Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Kasulu ameliagiza Baraza la Madiwani kuhakikisha changamoto zote zilizowasilishwa katika kikao hicho zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati, ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa miradi na kuboresha huduma kwa wananchi.
