Kasulu yasisitiza matumizi sahihi na marejesho ya mikopo ya 10%
Buha FM Radio

Kasulu yasisitiza matumizi sahihi na marejesho ya mikopo ya 10%

6 May 2026, 8:10 pm

Wananchi na wanufaika wa mikopo ya asilimia 10% waombwa kuitumia vizuri na kurejesha kwa wakati.

Na; Mwandishi wetu

Mwenyekiti wa Kamati ya Uhakiki wa Mikopo ya 10% na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kasulu, Theresia Mtewele, amevitaka vikundi vinavyoomba mikopo hiyo kuhakikisha vinaitumia kulingana na maandiko waliyowasilisha ili iweze kuleta tija na kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.

Ameyasema hayo wakati wa zoezi la uhakiki wa vikundi vilivyoomba mikopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, kwa lengo la kuthibitisha kama vinakidhi vigezo vya kunufaika na mikopo hiyo katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026.

Sauti ya Katibu Tawala.

Aidha, Katibu Mtewele amesisitiza umuhimu wa marejesho ya mikopo kwa wakati, akieleza kuwa nidhamu hiyo itawezesha vikundi vingine kupata fursa ya mikopo, pamoja na wanufaika waliopo kuwa na nafasi ya kuomba mikopo mikubwa zaidi katika siku zijazo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uhakiki wa Mikopo ya 10% na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kasulu, Theresia Mtewele, akiwa na wananchi na wanufaika wa mikopo ya 10% wilayani Kasulu.Picha na Mwandishi wetu.
Sauti ya Katibu Tawala.

Katika hatua nyingine, Theresia ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kwa usimamizi madhubuti wa utoaji wa mikopo hiyo inayotokana na 10% ya mapato ya ndani, pamoja na utaratibu mzuri wa utoaji elimu kwa wanufaika.

Mwakilishi wa Kamanda wa Polisi Wilaya ya Kasulu, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Willy Lupa, amesema mikopo hiyo inaakisi dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuyawezesha makundi mbalimbali katika jamii kujikwamua kiuchumi.

Sauti ya Kamanda wa Polisi Wilaya ya Kasulu, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Willy Lupa.

Mwakilishi wa Kamanda wa Polisi Wilaya ya Kasulu, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Willy Lupa, akizungumza mbele ya wanufaika wa mikopo ya 10% picha na Mwandishi wetu.

Kwa upande wake, Afisa Mwandamizi wa TAKUKURU Wilaya ya Kasulu, Alpha Eliatosha, amevitaka vikundi hivyo kuepuka kubadili malengo waliyojiwekea katika maandiko yao, akieleza kuwa hali hiyo mara nyingi husababisha kushindwa kurejesha mikopo kwa wakati.

Sauti ya Afisa Mwandamizi wa TAKUKURU Wilaya ya Kasulu, Alpha Eliatosha.

Naye Katibu wa Kamati hiyo, Victoria Makyao, amebainisha kuwa mafanikio ya mpango huo yanategemea nidhamu ya vikundi katika kutekeleza malengo yao na utayari wa kupokea na kufuata ushauri wa kitaalamu unaotolewa.

Sauti ya Katibu wa Kamati hiyo, Victoria Makyao.

Katika zoezi hilo, Kamati ilitembelea na kuhakiki vikundi vilivyopo katika kata za Makere, Nyachenda, Kigembe, Rusesa, Muzye, Kalela na Nyakitonto.

Baadhi ya wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu. Picha na Mwandishi wetu.