Buha FM Radio
Buha FM Radio
24 October 2026, 1:12 am

Kutokana na changamoto zinazowakabili baadhi wazee katika Halmashauri ya mji Kasulu mkoa wa Kigoma halmashauri imetumia zaidi ya shilingi milioni 17 kwa ajili ya kutoa msamaha wa matibabu kwa jumla ya wazee 1973 kwa kipindi cha robo ya mwaka kuanzia Julai hadi Septemba mwaka 2026.
Na; Emily Adam
Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma inaendelea na mpango wake wa kutoa msamaha na huduma ya matibabu bure kwa wazee katika vituo vyote vya afya na hospitali ikiwa ni jitaihada za kupunguza baadhi ya changamoto zinazowakabili wazee.
Hayo yamebainishwa na mratibu wa maswala ya wazee Afisa ustawi wa jamii wa halmashari ya mji Kasulu Yohana Atanas Mugaya wakati akizungumza na Buha FM na kueleza kuwa halmashauri hiyo imetumia zaidi ya shilingi milioni 17 kwa ajili ya kutoa msamaha wa matibabu kwa jumla ya wazee 1973 kwa kipindi cha robo ya mwaka kuanzia Julai hadi Septemba mwaka 2026.
Aidha ametoa wito kwa wazee kuhudhuria kwa wingi kwenye kliniki ya wazee ambayo hufanyika kila siku ya ijumaa katika Hospitali ya mji Kasulu, Mlimani kwa ajili ya uchunguzi wa afya zao na kufanyiwa vipimo vya mwili ili wapatiwe matibabu.

Katika hatua nyingine Afisa Mugaya ameongeza kuwa miongoni mwa changamoto zinazowakabili wazee wengi katika halmashauri hiyo ni pamoja na magonjwa, kutengwa na kunyanyapaliwa, kudhulumiwa malia zao pamoja na mambo mbalimbali.