Buha FM Radio
Buha FM Radio
27 October 2026, 4:01 pm

Wananchi wa Kitema na vijiji jirani wamepongeza upanuzi wa zahanati hiyo, huku wakiiomba Serikali kutatua changamoto ya maji na upungufu wa watoa huduma.
Na; Sharifat Shinji
Wananchi wa Kijiji cha Kitema na vijiji jirani katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma, wamenufaika na uboreshaji wa huduma za afya kufuatia upanuzi wa Zahanati ya Kitema uliogharimu shilingi milioni 222.1. Fedha hizo zilitolewa na Serikali kupitia uwekezaji katika huduma za afya ya mama na mtoto kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakazi wa vijiji vya Kitema na Mkieta, akiwemo Koleda Magata na Lazaro Magayane, wamesema uboreshaji huo umekuwa mkombozi kwa wananchi, hususan wajawazito ambao awali walilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya. Aidha, wameeleza kuwa ujenzi wa nyumba za watumishi utasaidia kuwafanya watumishi hao kuishi karibu na vituo vyao vya kazi.
Hata hivyo, Magayane amebainisha kuwa zahanati hiyo bado inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa watoa huduma za afya pamoja na ukosefu wa maji, akiiomba Wizara ya Afya na mamlaka husika kuchukua hatua za kutatua changamoto hizo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kitema, Abraham Ntebanyi, amesema wananchi wananufaika na ujenzi wa jengo la kliniki ya Baba, Mama na Mtoto pamoja na upanuzi wa chumba cha kujifungulia. Amesema maboresho hayo yamesaidia kupunguza changamoto ya baadhi ya huduma kutolewa katika mazingira yasiyofaa.
Naye Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kitema, Ezikiel Lawrence, amesema fedha zilizotolewa zilitumika kujenga nyumba mbili za watumishi, jengo la kliniki ya Baba, Mama na Mtoto, jengo la kujifungulia pamoja na kupanua jengo la wagonjwa wa nje (OPD). Ameeleza kuwa mradi huo ulianza kutekelezwa Novemba 21, 2025, na umekamilika kwa asilimia 100.

Kwa ujumla, upanuzi wa Zahanati ya Kitema unatarajiwa kuendelea kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wakazi wa Kitema na vijiji jirani, kwa kupunguza adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma katika maeneo ya Nyamunyusi na Kabanga, huku ukiboresha mazingira ya kujifungulia na kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto.

