Buha FM Radio
Buha FM Radio
26 October 2026, 6:17 pm

Kutokana na wanaume wengi kukwepa kuambatana na wenza wao kliniki wakati wa ujauzito, baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma wametaja hofu kuhusu hali zao za afya na majukumu ya uzalishaji kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia hali hiyo.
Na; Sharifat Shinji
Baadhi ya wananchi katika Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma, wametaja hofu ya kutokujiamini kuhusu hali zao za afya na majukumu ya uzalishaji yanayokinzana na muda wa kliniki kuwa miongoni mwa sababu zinazowafanya baadhi ya wanaume kushindwa kuambatana na wenza wao kliniki wakati wa ujauzito.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wengine, Chrispin Philibet, mkazi wa Kata ya Kagerankanda, Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, amesema baadhi ya wanaume wenye mahusiano na wanawake zaidi ya mmoja hukabiliwa na hofu ya kutokujiamini kuhusu hali zao za afya, jambo linaloweza kuwafanya kusita kuambatana na wenza wao kliniki kwa ajili ya kufanyiwa vipimo wakati wa ujauzito.
Aidha, amewaomba wataalamu wa afya kuongeza elimu kwa wanaume kuhusu umuhimu wa kuhudhuria kliniki pamoja na wenza wao, huku akiwahimiza kushiriki katika vipimo vya magonjwa mbalimbali na kufuatilia maendeleo ya mtoto aliye tumboni, akieleza kuwa hatua hiyo inaweza kusaidia kujenga amani na kuimarisha mahusiano katika familia.
Kwa upande wake, Josephina Dawichi, muuguzi na mtoa huduma za afya katika Zahanati ya Kata ya Kagerankanda, amesema wahudumu wa afya huwashauri wajawazito kuwashawishi wenza wao kuambatana nao kliniki wanapofikisha miezi mitatu ya ujauzito ili kufuatilia maendeleo ya mtoto na hali ya afya ya mama.
Hata hivyo, ushiriki wa wanaume katika kliniki za wajawazito unaendelea kuwa muhimu katika kuhakikisha afya na usalama wa mama na mtoto wakati wa ujauzito, huku elimu zaidi ikihitajika kuondoa hofu na vikwazo vinavyowafanya baadhi yao kushindwa kuambatana na wenza wao kliniki.