Buha FM Radio

Serikali yawaangukia wananchi kukamilisha miradi ya maendeleo Kagerankanda

23 October 2026, 8:10 pm

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Kagerankanda wakiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata hiyo. Picha na Ajomba Lukumba.

Kutokana na changamoto mbalimbali za miundombinu, serikali imewaelekeza wananchi wa Kata ya Kagerankanda, Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, kuchangia asilimia 20 ya nguvu kazi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, katani hapo.

Na; Sharifat Shinji

Wananchi wa Kata ya Kagerankanda, Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, wametakiwa kushiriki kikamilifu katika miradi ya maendeleo kwa kuchangia asilimia 20 ya nguvu kazi katika ujenzi wa Soko la Sofya na miundombinu ya vyoo katika shule mbalimbali za kata hiyo.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata hiyo, Afisa Mtendaji wa Kata ya Kagerankanda Bunyukwa Makinga amesema ujenzi wa banda la Soko la Sofya unagharimu jumla ya shilingi milioni 54, fedha zinazotolewa na wadau mbalimbali wa maendeleo. Ameeleza kuwa wananchi wanapaswa kuchangia kwa ukusanyaji wa mawe yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni moja.

Sauti ya Afisa mtendaji kata ya Kagerankanda Makinga.

Aidha, kuhusu ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule mbalimbali za kata hiyo, Makinga amewataka wananchi kushiriki kwa kuchimba matundu ya vyoo pamoja na kukusanya mawe mawili kutoka kila kaya ili kusaidia kukamilisha ujenzi wa miundombinu hiyo.

Sauti ya Afisa mtendaji kata ya Kagerankanda Makinga.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Kagerankanda, Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, Banyukwa Makinga akiwa katika mkutano wa hadhara. Picha na Ajomba Lukumba.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Kata ya Kagerankanda wameipokea miradi hiyo na kuahidi kushiriki katika utekelezaji wake kwa kutoa michango inayohitajika. Hata hivyo, wameiomba serikali ya kata hiyo kuhakikisha baadhi ya miradi inakamilishwa bila kutegemea michango ya wananchi.

Sauti za wananchi.
Baadhi ya wananchi wa Kata ya Kagerankanda wakiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata hiyo. Picha na Ajomba Lukumba.

Kata ya Kagerankanda ni miongoni mwa kata zinazounda Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, ambapo ushiriki wa wananchi katika miradi ya maendeleo unatarajiwa kusaidia kuboresha miundombinu na kuongeza upatikanaji wa huduma bora za kijamii.