Buha FM Radio

Tuyabebe Masikitiko yajenga nyumba 18 zawenye uhitaji Kasulu

25 November 2026, 7:27 pm

Mnufaika wa mradi wa ujenzi wa nyumba, Elizabeth Kachila akiwa na baadhi ya viongozi wa kikundi na sertekali wakati wa zoezi la uendelezaji wa ujenzi wa nyumba yake katika kijiji cha Kalimongoma kata ya Makere. Picha na Sharifat Shinji.

Kutokana na hali ngumu ya maisha kwa baadhi ya wakazi wa vijiji mbalimbali nchini, wadau wa maendeleo wilayani Kasulu wamefanikiwa kujenga nyumba 18 kwa wananchi wanaoishi katika mazingira magumu na wenye uhitaji.

Na: Sharifat Shinji

Kikundi cha kujitolea cha Tuyabebe Masikitiko kilichopo Kata ya Makere, Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, kimefanikisha ujenzi wa nyumba 18 kwa ajili ya wananchi wanaoishi katika mazingira magumu wilayani humo, huku kikiendeleza kampeni ya Kasulu Bila Nyumba za Nyasi Inawezekana.

Akizungumza wakati wa kuendelea kwa ujenzi wa nyumba ya mkazi mmoja wa Kijiji cha Kalimongoma, Mwenyekiti wa kikundi hicho, Daniel Bakunda, amesema kuwa kikundi kinaendelea kutekeleza malengo yake ya kuwapatia makazi bora wananchi wanaoishi katika mazingira magumu kwa gharama nafuu, kupitia ushirikiano kutoka serikalini.

Sauti ya Daniel Bakunda.
Kushoto ni Mwenyekiti wa Kikundi cha Tuyabebe Masikitiko Daniel Bakunda akimkabizi mwenyekiti wa Halmashauri Samweli Kadogo nyaraka za utekerezaji wa miradi. Picha na Sharifat Shinji.

Aidha, Bakunda amesema kuwa kupitia kikundi hicho wanaendelea na kampeni ya kutokomeza makazi duni kwa wakazi wa Wilaya ya Kasulu bila ubaguzi, huku akiwataka wadau na wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi hizo.

Sauti ya Daniel Bakunda.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Samweli Kadogo, amesema halmashauri imekuwa mdau muhimu katika kufanikisha juhudi za kikundi hicho kwa kukipatia ushirikiano pale kinapowasilisha maandiko ya miradi yake.

Sauti ya Samweli Kadogo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Samweli Kadogo pamoja na Mwenyekiti wa Kikundi cha Tuyabebe Masikitiko Daniel Bakunda wakati ya shughuri ya uendelezaji ujenzi wa nyumba. Picha na Sharifat Shinji.

Ameongeza kuwa serikali za vijiji zimekuwa zikichangia upatikanaji wa viwanja kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hizo na ametowa wito kwa wananchi kushiriki katika zoezi la kuboresha makazi ya Wilaya ya Kasulu. 

Sauti ya Samweli Kadogo.

Naye mnufaika wa kampeni hiyo, Elizabeth Kachila, ambaye ana changamoto ya ulemavu wa viungo, amekishukuru kikundi hicho kwa kuwezesha ujenzi wa nyumba yake. Hata hivyo, ameiomba serikali kuendelea kumsaidia katika malezi na elimu ya watoto wake, wakiwemo wanafunzi wanaoendelea na masomo ya chuo kikuu na mwingine anayetarajia kujiunga na kidato cha kwanza Januari 2027.

Sauti ya Elizabeth Kachila.
Mnufaika wa mradi wa ujenzi wa nyumba, Elizabeth Kachila akiwa na baadhi ya viongozi wa kikundi na sertekali wakati wa zoezi la uendelezaji wa ujenzi wa nyumba yake katika kijiji cha Kalimongoma kata ya Makere. Picha na Sharifat Shinji.

Kikundi cha Tuyabebe Masikitiko kilianzishwa mwaka 2017 kikiwa na wanachama 17, kwa lengo la kuwasaidia wananchi wanaoishi katika mazingira magumu, na hadi sasa kimefanikisha kujwafikia wakazi 18 wakiwemo watu wenye ulemavu, wajane, yatima, wazee na watu wote wanaotoka katika mazingira magumu, kupitia kampeni yake ya Kasulu Bila Nyumba za Nyasi Inawezekana.