Radio Kwizera

Changamoto ya umeme yatajwa kikwazo kwa maendeleo Geita

April 28, 2026, 7:25 pm

Baadhi ya Viongozi na wadau wakiwa katika Viwanja vya Dkt Samia Geita katika maandalizi kuelekea maonesho ya Wakandarasi, Wajenzi na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara. Picha na Clment Shawishi

Wizara ya Viwanda na Biashara inawapa kipaumbele wawekezaji binafsi kukuza uchumi na kwamba huduma ya Nishati haina budi kuimarishwa kuwezesha uwekezaji huo

Na Clement Shawishi – GEITA

Shirika la Usambazaji Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Geita limeombwa kushughulikia changamoto ya upatikanaji wa umeme Mkoani humo ili shughuli za uzalishaji zipige hatua.

Rai hiyo imetolewa leo na Afisa Maendeleo ya Biashara kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara Bi Anneth Ngoyi wakati akizungumza na wanahabari kuelekea ufunguzi wa maonesho ya Wakandarasi, Wajenzi na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara viwanja vya maonesho vya Dkt Samia mjini Geita.

Bi Anneth amesema Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara inawapa kipaumbele wawekezaji binafsi kukuza uchumi na kwamba huduma ya Nishati haina budi kuimarishwa kuwezesha uwekezaji huo.

Maonesho ya Wakandarasi, Wajenzi na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara yanatarajiwa kufunguliwa rasmi na Waziri wa Viwanda na Biashara Bi Judith Kapinga Aprili 29 mwaka huu katika viwanja vya Dkt Samia mjini Geita.