Radio Kwizera
Radio Kwizera
July 7, 2025, 8:53 pm

Vikundi 6 ni vya wanawake ambavyo vimekopeshwa shilingi milioni 159, vikundi vya Vijana 5 vimekopeshwa shilingi milioni 132.5 huku kikundi kimoja cha wanawake ambacho kimekopeshwa jumla ya shilingi milioni 50 kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa zinazotokana na maziwa.
Na Shafiru Yusuph- Muleba, Kagera
Jumla ya ng`ombe 44 zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 340 zimegawiwa kwa vikundi vya wafugaji 11 vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera kwa ajili ya uzalishaji na usindikaji wa maziwa.
Akizungumza wakati wa zoezi la ugawaji wa mifugo hiyo liliyofanyika katika Kata ya Mubunda Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Bw. Evart Kagaruki amesema kuwa fedha hizo zimetolewa kwa kupitia asilimia 10 za mapato ya ndani bila riba.
Bwana Kagaruki amesema kuwa vikundi 6 ni vya wanawake ambavyo vimekopeshwa shilingi milioni 159, vikundi vya Vijana 5 vimekopeshwa shilingi milioni 132.5 huku kikundi kimoja cha wanawake ambacho kimekopeshwa jumla ya shilingi milioni 50 kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa zinazotokana na maziwa.

Amesema kuwa mradi huu wa ng`ombe wa maziwa umeenda sambamba na uchakataji wa zao la maziwa ili kuongeza thamani ya zao hilo, kuwajengea uwezo wafugaji kufuga kisasa, kuzalisha maziwa bora na kupata masoko ya uhakika.
Aidha Bw. Kagaruki amewataka wafugaji hao kuhakikisha mifugo hiyo inatunzwa kadri ya makubaliano yalivyo andikwa kwenye mradi na kwmaba marejesho yafanyike kila mwezi kwa mujibu wa mkataba.
Awali Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Muleba Bi. Edna Kabyazi amesema ng`ombe hao ni aina ya Friesian mmoja ana uwezo wa kutoa maziwa lita 20 kwa siku ambapo kwa mwaka anazalisha lita 7,300 na kuzaa mara tano hadi saba kwa kipindi chote cha maisha yake.
Bi. Edna Kabyazi amesema kuwa vikundi vyote vilivyopatiwa mifugo hiyo tayari vimepatiwa mafunzo juu ya ufugaji wa kisasa wenye tija, haki, wajibu na majukumu yao pamoja na namna ya kushirikiana na maafisa mifugo juu ya usimamizi wa mradi huo.
Aidha tangu dirisha la mikopo lifunguliwe Halmashauri ya Wilaya ya Muleba imetoa mkopo wa zaidi ya shilingi bilioni 2, na milioni 883 kwa vikundi 152.