Radio Kwizera

Geita yang’ara kiuchumi kupitia sekta ya madini, uwekezaji

April 20, 2026, 7:26 pm

Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela akizungumza wakati wa mkutano mkuu wa kawaida wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Geita. Picha na Clement Shawishi

Uwekezaji katika sekta ya madini umechangia pakubwa sekta hiyo kuongeza pato la Mkoa wa Geita ambalo kwa sasa ni zaidi ya Shilingi Trillion 9 kwa mwaka.

Na Clement Shawishi- GEITA

Imeelezwa kuwa zaidi ya 40% ya uzalishaji wa dhahabu Mkoani Geita inatokakana na wachimbaji wadogo ambao mwitikio wao kupata leseni za uchimbaji umekuwa mkubwa.

Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela amesema hayo wakati akiwasilisha hali ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo Mkoani humo kwenye mkutano mkuu wa kawaida wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Geita

Shigela amesema kuwa uwekezaji katika sekta ya madini umechangia pakubwa sekta hiyo kuongeza pato la Mkoa wa Geita ambalo kwa sasa ni zaidi ya Shilingi Trillion 9 kwa mwaka

Mwenyekiti wa Wachimbaji Madini Mkoa wa Geita Bw, Titus Charles Kabuo amesema mwitikio wa wachimbaji kutafta leseni katika maeneo ya shughuli zao kumepunguza migogoro ya ardhi na kuwaongezea kipato

Kwa niaba ya Wabunge wa majimbo ya Mkoa wa Geita Naibu Waziri Mkuu Msitaafu na Mbunge wa Jimbo la Bukombe Mkoani Geita Dkt Dotto Mashaka Biteko amesema ushirikiano miongoni mwa Watumishi wa Umma ni njia sahihi kuendelea kukuza uchumi wa Mkoa huo

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Bw, Jumanne Misungwi kwa niaba ya madiwani wote Mkoani humo amesema kila Kata yenye shughuli za uchimbaji itawapa kipaumbele Vijana ambao kwa kiasi kikubwa ndiyo hufanya shughuli za uchimbaji madini.