Radio Kwizera

Vyombo vya sheria vyapewa mafunzo kukabili uharibifu wa misitu

April 20, 2026, 7:10 pm

Miongoni mwa Maafisa wa Jeshi la Uhifadhi TFS na Polisi walipotembelea eneo la Hifadhi ya Msitu wa Nyantakara, Nyakanazi Biharamulo. Picha na William Mpanju

Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa TFS Kanda ya Ziwa, Ebrandino Mgiye, amesisitiza kuwa utoaji wa elimu kwa wananchi ni nyenzo muhimu katika kupunguza vitendo vya uhalibifu wa misitu.

Na William Mpanju- Biharamulo, Kagera

Maafisa wa Jeshi la Uhifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wilayani Biharamulo wameeleza kuridhishwa kwao na mafunzo waliyopokea kuhusu matumizi ya ndege nyuki (drone), teknolojia inayosaidia kufuatilia na kubaini vitendo vya uhalibifu wa mazingira pamoja na shughuli zisizo halali ndani ya hifadhi za misitu.

Matumizi ya drone hiyo tayari yameanza kuonyesha mafanikio, baada ya kubaini baadhi ya wananchi wanaojihusisha na shughuli za kibinadamu ndani ya maeneo ya hifadhi kinyume cha sheria.

Sambamba na hilo, wadau mbalimbali wa sekta ya sheria wakiwemo maafisa wa Polisi, Waendesha Mashitaka na Wanasheria wa Serikali wamepatiwa mafunzo maalum kuhusu namna ya kushughulikia kesi za uhalibifu wa misitu, pamoja na hatua za kisheria zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa.

Akizungumza katika eneo la Nyakanazi wilayani humo, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa TFS Kanda ya Ziwa, Ebrandino Mgiye, amesisitiza kuwa utoaji wa elimu kwa wananchi ni nyenzo muhimu katika kupunguza vitendo vya uhalibifu wa misitu.

Alifafanua kuwa vitendo kama uchomaji wa mkaa, ukataji wa kuni na uvunaji holela wa mazao ya misitu vinaendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo kuongezeka kwa ukame, hivyo hatua za kisheria zinapaswa kuchukuliwa kwa haraka dhidi ya wahusika.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mashitaka Mkoa wa Kagera, Magreth Mwaseba, ameeleza kuwa Mahakama zitaendelea kushirikiana na vyombo vingine vya dola kuhakikisha haki inatendeka kwa wanaokiuka sheria kwa kuingia na kufanya shughuli zisizo halali ndani ya hifadhi za misitu.