Radio Kwizera

Madiwani na Watumishi kuchangia elfu 12 za taka

May 12, 2026, 9:38 am

Baadhi ya watumishi wa Manisapaa ya Bukoba waliohudhuria Baraza la Madiwani wilayani Bukoba. Picha na Enock Yoronimo

‎Pendekezo hilo la kutoa shilingi 1,000 kila mwezi kama ada ya taka limetolewa na Meya Acton Rwankomezi kutokana na kutozolewa taka kwa wakati kutokana na ukosefu wa magari ya kutosha kubeba taka

Na Enock Yoronimo- Bukoba, KAGERA

Kutokana na changamoto ya uchelewaji wa uzowaji wa taka katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera Baraza la madiwani katika manispaa hiyo limependekeza kutoa kiasi cha Tsh 12,000 kwa kila diwani na watumishi ili kuonyesha jitihada kwa Wananchi katika uchangiaji wa ada ya taka kila mwezi.

‎Pendekezo hilo la kutoa shilingi 1,000 kila mwezi kama ada ya taka limetolewa na Meya Acton Rwankomezi kutokana na kutozolewa taka kwa wakati kutokana na ukosefu wa magari ya kutosha kubeba taka hali iliyowafanya wananchi kuacha kuchangia ada ya taka.

‎Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango miji na Mazingira Eliud Kahabuka wakati akiwa katika kikao cha Baraza la madiwani amesema ulipaji fedha ya taka ni bora uanzie kwa watumishi wa Manispaa na madiwani ili iweze kuonyesha hamasa kwa wananchi.

‎Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba Jacob Nkwera amesema fedha za gari ya taka zipo na utaratibu wa kufanya matengenezo unaendelea huku timu ya maafisa afya na watendaji ikiundwa ili iweze kufanya ufuatiliaji wa jambo hilo ili mji wa Bukoba uweze kuwa safi.