Radio Kwizera
Radio Kwizera
April 29, 2026, 1:40 pm

Elimu hiyo kwa wanafunzi wa shule za msingi inajenga kizazi chenye uelewa wa mapema kuhusu tahadhari za majanga ya moto
Na Clement Shawishi- GEITA.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita limeendelea kutoa elimu kwa wanafunzi wa Shule za Msingi juu ya namna ya kujilinda dhidi ya ajali na matukio ya moto majumbani na shuleni.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita, Mrakibu Msaidizi (ASF) Keneth Angolwisye Mwakasitu ameongoza utoaji elimu hiyo leo katika Shule ya Msingi Mseto na Shule ya Msingi Bombambili Manispaa ya Geita.
Amesema elimu hiyo kwa wanafunzi wa shule za msingi inajenga kizazi chenye uelewa wa mapema kuhusu tahadhari za majanga ya moto na kwamba tayari jeshi limeanzisha klabu za zimamoto katika baadhi ya shule ili kuendeleza juhudi hizo.
Balozi wa Zimamoto Mwalimu Yusufu Hamisi Ibrahim, amesema awali elimu ya zimamoto haikupewa kipaumbele hivyo kusababisha Jamii nyingi kukosa uelewa wa namna ya kujikinga dhidi ya majanga ya moto na mafuriko
Kwa niaba ya wanafunzi wote, Mwanafunzi Aloyce Alexanda amesema mafunzo hayo yatawasaidia kuyatumia maarifa waliyopata shuleni na majumbani kwao, na hivyo kuwa sehemu ya suluhisho katika kupunguza ajali za moto
Elimu hiyo ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya siku ya Zimamoto Ulimwenguni ambayo huadhimishwa kila ifikapo Mei 4 ya kila mwaka.