Radio Kwizera

WEO Busunzu, Kibondo awataka watumishi kuzingatia sheria

April 28, 2026, 3:42 pm

Baadhi ya Viongozi wa Kata ya Busunzu wilayani Kibondo, mkoani Kigoma wakiwa katika picha ya pamoja baada ya ziara maalumu kwenye taasisi za elimu na afya. Picha na Samwel Masunzu

Watumishi wanatakiwa kuwa kiunganishi kati ya serikali na wananchi hali itakayosaidia kuepusha wananchi kuichukia serikali pamoja na viongozi.

Na Samwel Masunzu- Kibondo, KIGOMA

Afisa Mtendaji wa kata ya Busunzu wilayani Kibondo mkoani Kigoma Bw. Shedrack Totoye amewataka watumishi wa Umma ndani ya kata hiyo kuhakikisha wanafanya kazi kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma ili kuepusha malalamiko na migogoro kutoka kwa wananchi.

Bw. Totoye amesema hayo wakati wa ziara maalumu kwenye taasisi za elimu na afya ambapo ameanza na Zahanati ya Kijiji cha Kisogwe na kukutana na wenyeviti wa vitongoji, kamati ya afya ya zahanati, viongozi wa kijiji na wataalamu wa zahanati hiyo, pamoja na diwani wa kata

Amesema kanuni na sheria za utumishi wa umma zinakataza watumishi kuwa sehemu ya migogoro katika maeneo ya kazi

Aidha amesisitiza kila mmoja kuepuka lugha chafu wakati wa kutoa huduma na kusimamia miongozo inayotolewa na serikali hasa katika utoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto waliopo chini ya umri wa miezi 3 na kwamba ni marufuku mwananchi kutengenezewa viashiria vya rushwa katika kupata huduma za matibabu

Naye diwani wa kata ya Busunzu Bw. Giles Kagoma amewataka watumishi kuwa kiunganishi kati ya serikali na wananchi hali itakayosaidia kuepusha wananchi kuichukia serikali pamoja na viongozi.

Katika ziara hiyo pia mkaguzi wa Polisi kata ya Busunzu Afande Mfaume amesisitiza kila mmoja kuendelea kuwajibika katika ulinzi na usalama.