Radio Kwizera

Polisi Kigoma wavunja mtandao wa uhalifu kwa msako mkoa mzima

April 21, 2026, 3:46 pm

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Kigoma Philimoni Makungu akionesha miongoni mwa vitu vya wizi vilivyokamatwa katika doria iliyofanyika mkoani humo. Picha na Naomi Milton

Katika maeneo ya Mnanila, Manyovu wilayani Buhigwe Askari Polisi walifanikiwa kuwakamata watu wawili wa tukio la mauaji na unyang’anyi wa pikipiki kwa bodaboda aliyeuwawa hivi karibuni

Na Naomi Milton

Jeshi la Polisi mkoani Kigoma katika misako na operesheni mbalimbali zinazoendelea katika wilaya zote za mkoa limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa kwa makosa mbalimbali ikiwemo wizi, mauaji, bangi na wahamiaji haramu.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Kigoma Philimoni Makungu amesema watu watatu walikamtwa wakiwa na vyuma 30 vya miundombinu ya reli katika kijiji cha Mpeta wilayani Uvinza huku watano wakikamtwa kwa wizi wa sola saba mali idhaniwayo kuwa ya mradi wa maji kijiji cha Kabingo.

Ameongeza kuwa mnamo Aprili 4, 2026 katika maeneo ya Mnanila, Manyovu wilayani Buhigwe Askari Polisi walifanikiwa kuwakamata watu wawili wa tukio la mauaji na unyang’anyi wa pikipiki kwa bodaboda aliyeuwawa hivi karibuni ambapo watuhumiwa watafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika.

Sambamba na hayo watuhumiwa 7 wamekamatwa wakiwa na bangi gunia mbili na kete 23 na mtu mmoja kuteketezewa shamba la bangi lenye ukubwa wa hekari 6 katika wilaya ya Kasulu.

Hata hivyo Kamanda Makungu amewataka wananchi kutoa taarifa pale wanapoona vitendo vya uhalifu ili kuendelea kuuweka mkoa katika hali ya amani na utulivu.