Radio Kwizera

Askofu Kasala atabaruku kanisa jipya Sengerema

October 15, 2026, 8:19 pm

Kanisa jipya la Parokia ya Yesu Kristu Mfalme Sengerema mjini lililotabarukiwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita Mhashamu Askofu Flavian Matindi Kasala. Picha na Clement John

Kanisa hilo jipya ambalo ujenzi wake umegharimu bil 1.6 umekamilika na kukidhi vigezo vya kutumika kama Kanisa Kuu la Parokia kulingana na utaratibu wa Liturujia ya Kanisa Katoliki.

Clement Shawishi– Sengerema, MWANZA.

Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita Mhashamu Askofu Flavian Kasala Kanisa jipya la Parokia ya Yesu Kristu Mfalme Sengerema mjini akitoa wito kwa Jamii, Walei na Viongozi wa Kanisa kulinda miundombinu ya Kanisa.

Mhashamu Baba Askofu Kasala ametoa wito huo katika homilia yake wakati wa ibaada ya Misa Takatifu maalum kwa kutabaruku Kanisa hilo jipya ambalo ujenzi wake umekamilika na kukidhi vigezo vya kutumika kama Kanisa Kuu la Parokia kulingana na utaratibu wa Liturujia ya Kanisa Katoliki.

Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita Mhashamu Askofu Flavian Kasala (aliyepiga magoti) akitabaruku kanisa jipya la Parokia ya Yesu Kristu Mfalme Sengerema mjini. Picha na Clement John

Paroko wa Parokia hiyo Padre Edison Nduha amepongeza jitihada za Walei na Waamini wengine kufanikisha ujenzi wa Kanisa hilo ambalo limegharimu Bilioni 1.6 likiwa na uwezo wa kuchukua Watu elfu 1 na 600 kwa pamoja.

Kwa niaba ya Serikali, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza Bi. Seni Nganga amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Taasisi za Dini kulinda Maadili, amani, utoaji wa huduma za kijamii hususani Elimu, Afya, Maji na ulinzi na usalama kila mahali.

Parokia ya Yesu Kristu Mfalme Sengerema mjini ni miongoni mwa Parokia zaidi ya 30 zinazounda Jimbo Katoliki la Geita ambayo ujenzi wa Kanisa lake jipya ulianza Machi 2015 na kusimamiwa na Mapadre waliowahi kuihudumia kwa nyakati tofauti, Walei na Waamini wa maeneo mbalimbali mpaka kukamilika kwake Oktoba 13 mwaka huu 2026.

Baadhi ya Viongozi wa Dini na Waumini wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kutabarukiwa kwa Kanisa jipya la Parokia ya Yesu Kristu Mfalme Sengerema mjini. Picha na Clement John
Baadhi ya waumini waliohudhuria Misa ya kutabarukiwa kwa Kanisa jipya la Parokia ya Yesu Kristu Mfalme Sengerema mjini. Picha na Clement John