Radio Kwizera
Radio Kwizera
October 9, 2026, 1:56 pm

Pamoja na mafanikio yaliyopatikana, bado kuna changamoto zinazohitaji kupewa kipaumbele ili kuboresha ustawi wao.
Na Enock Yoronimo- Missenyi, KAGERA.
Wazee wilayani Missenyi mkoani Kagera wameiomba Serikali kuboresha huduma za afya na kushughulikia changamoto zinazowakabili ili waweze kupata huduma bora na kuishi katika mazingira salama na yenye heshima.
Wakizungumza mbele ya Viongozi wa serikali ya Wilaya hiyo katika Kijiji cha Byeju, Kata ya Mutukula, wazee hao wamesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana, bado kuna changamoto mbalimbali zinazohitaji kupewa kipaumbele ili kuboresha ustawi wao.
Wazee hao wamesema ni muhimu sana kuweka mazingira bora na mipango mahsusi ya kuboresha huduma na ustawi wao hususani katika sekta ya afya, hali ya maisha kiuchumi, ulinzi na usalama pamoja na ushirikishwaji katika masuala ya maendeleo
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Mwanaidi Mang’uro, amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wazee, ikiwemo kuboresha huduma za afya na kushughulikia changamoto za matibabu pamoja na msamaha wa gharama za matibabu kwa kundi hilo.
Aidha, Mang’uro amewataka wazee kutumia uzoefu wao kuwaelimisha vijana kuhusu umuhimu wa kulinda amani na utulivu wa Taifa, akisisitiza nafasi yao katika kujenga jamii yenye mshikamano na maadili mema.

