Radio Kwizera
Radio Kwizera
November 13, 2026, 8:36 am

Miradi iliyoathirika ni pamoja na ujenzi wa Soko la Kimataifa la Kagunga na jengo la Utawala la Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Na Naomi Milton- KIGOMA.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kigoma imefanikiwa kurejesha jumla ya Shilingi milioni 320.9 zilizokuwa zimepotea kutokana na vitendo vya ubadhirifu na ukiukwaji wa taratibu za usimamizi wa fedha za umma katika kipindi cha Aprili hadi Sept 2026.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kigoma John Mgallah amesema kati ya fedha hizo Shilingi milioni 260.1 zimerejeshwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji na Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kufuatia kubainika kwa mkandarasi wa kampuni ya GOPA CONTRACTORS TANZANIA LIMITED kutelekeza miradi ya maendeleo baada ya kupokea fedha za malipo ya awali.
Amesema miradi iliyoathirika ni pamoja na ujenzi wa Soko la Kimataifa la Kagunga na jengo la Utawala la Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji ambapo kupitia jitihada za TAKUKURU za kumtafuta na kumrejesha mkandarasi huyo fedha hizo zimefanikiwa kurejeshwa katika akaunti za benki za halmashauri husika.
Aidha Mgallah amesema katika kipindi hicho TAKUKURU imefanikiwa kurejesha Shilingi 230,000 kwa wananchi na Shilingi milioni 60.4 zilizorejeshwa Serikalini akisisitiza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za taasisi hiyo kuhakikisha fedha za umma zinalindwa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.