Radio Kwizera

Tanzania yapokea wakimbizi 11,049 toka DRC ndani ya miezi mitano

July 3, 2023, 12:43 pm

Mkurugenzi idara ya huduma kwa wakimbizi nchini Tanzania Bw. Suddy Mwakibisa amesema serikali ya Tanzania imepokea  waomba hifadhi  11,049 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa kipindi cha mwezi Januari hadi  Mei 30 2023.

Mkurugenzi idara ya huduma kwa wakimbizi Tanzania (aliye vaa miwani) Bw. Suddy Mwakibisa akizungumza na baadhi ya wakimbizi wa kambi ya Nyarugusu wilalayani Kasulu mkoani Kigoma.

Na; Amina Semagogwa

Serikali ya Tanzania  kupitia kambi ya wakimbizi Nyarugusu  imepokea  jumla ya waomba hifadhi  11,049 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa kipindi cha mwezi Januari hadi  Mei 30, 2023.

Mkurugenzi idara ya huduma kwa wakimbizi nchini Tanzania Bw. Suddy Mwakibisa amesema idadi hiyo  ya wakimbizi  kutoka  DRC kuingia nchini Tanzania  inatokana na machafuko yanayoendelea  nchini  kwao.

Amesema hayo wakati akihutubia umati wa wakimbizi kwenye maadhimisho ya siku ya Mkimbizi Duniani hivi karibuni ambayo kitaifa yamefanyika katika kambi wakimbizi Nyarugusu wilayani Kasulu mkoani Kigoma.

Bw. Mwakibisa amesema  kuanzia mwezi January hadi Mei ,2023  jumla ya wakimbizi 1,343 kutoka familia 527 wamerudi nchini  Burundi  kwa  hiari.

Mkurugenzi idara ya huduma kwa wakimbizi nchini Tanzania Bw. Suddy Mwakibisa akiwa hutubia wakimbizi katika kambi ya Nyarugusu wilayani Kasulu mkoani Kigoma.

Bw. Mwakibisa amesema Tanzania imekuwa ikipokea wakimbizi kwa miaka mingi na kwamba  hadi kufikia sasa kambi za wakimbizi Nduta na Nyarugusu zina zaidi  ya wakimbizi 260,000.

Sehemu ya umati wa wakimbizi wakimsikiliza Mkurugenzi idara ya huduma kwa wakimbizi nchini Tanzania Bw. Suddy Mwakibisa.

Ikumbukwe kuwa  Juni 20 mwaka  huu ilikuwa na siku ya Mkimbizi Duniani ambayo kitaifa imeadhimishwa katika kambi ya wakimbizi Nyarugusu wilayani Kasulu mkoani Kigoma ikiwa na Kauli mbiu ya  ‘’ Matumaini mbali na nyumbani,  ulimwengu unaojumuisha  wakimbizi kila wakati’’.