Radio Kwizera
Radio Kwizera
May 2, 2026, 3:15 pm

Elimu ya lishe inatakiwa kuwafikia wananchi wote ili wajue umuhimu wa kutunza afya zao na kupima mara kwa mara
Na Enock Yoronimo- Bukoba, KAGERA
Mkuu wa wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, Erasto Sima amesema upo umuhimu wa kutoa huduma bora na kwa wakati kwenye vituo vyote vya afya zikiwemo huduma za Elimu ya lishe kwa wananchi.
Ametoa wito huo wakati akiongoza kikao cha tathimini ya mkataba wa usimamizi wa afua za lishe pamoja na kujadili utekelezaji wa shughuli za lishe kwa kipindi cha robo ya tatu ya 2025/2026, kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya Bukoba mkoani humo.
Sima amesema elimu ya lishe inatakiwa kuwafikia wananchi wote ili wajue umuhimu wa kutunza afya zao na kupima mara kwa mara ambapo wananchi wa Halmashauri ya wilaya ya Bukoba wametakiwa kutumia fursa ya kuwepo Kwa zahanati za Rugaze, Katoma, Kyamarenge, Kashozi na Rwamulumba kupima Afya zao.
Aidha Sima amewapongeza watumishi kwa utendaji wao mzuri kwenye maeneo yao, na kutoa zawadi kwa waganga wafawidhi na watendaji wa kata waliofanya vizuri katika utekelezaji wa afua za lishe kwa kipindi cha robo ya tatu ambapo kata ya Butelankuzi imeongoza kwa asilimia mia moja.