Radio Kwizera
Radio Kwizera
May 1, 2026, 10:16 pm

Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Burundi pamoja na Mashirika ya kimataifa, wamefanikiwa kuwarejesha jumla ya wakimbizi 165,494 kwa hiyari.
Na Michael Mpunije- Kibondo, KIGOMA.
Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi imefunga rasmi Kambi ya wakimbizi ya Nduta iliyopo wilayani Kibondo Mkoani Kigoma ambayo ilikuwa inahifadhi wakimbizi kutoka nchini jirani ya Burundi ikiwa ni baada ya wakimbizi hao kurejea katika nchi yao kwa hiyari.
Kambi hiyo ilikuwa imehifadhi zaidi ya wakimbizi laki moja kutoka nchini Burundi ambao kwa sasa wamerejeshwa kwenye nchi yao kufuatia hali ya amani na utulivu kuendelea kuimarika.
Waziri wa mambo ya Ndani ya Nchi Patrobas Katambi katika Hotuba yake wakati wa kufunga kambi hiyo amewataka watanzania kutathmini athari za maisha ya ukimbizi hatua itakayo saidia kuendelea kulinda amani ya nchi.
Aidha, amesema Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Burundi pamoja na Mashirika ya kimataifa, ikiwemo Shirika la kuhudumia wakimbizi la UNHCR wamefanikiwa kuwarejesha jumla ya wakimbizi 165,494 kwa hiyari kutokana na kuimarika kwa hali ya amani na utulivu katika nchi hiyo.
Wakati wa zoezi la kufunga kambi hiyo ya Nduta Viongozi mbalimbali akiwemo Mkurugenzi wa Idara ya huduma kwa Wakimbizi nchini Tanzania Sudi Mwakibasi na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro wamesisitiza kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Burundi kwa kudumisha amani, upendo na mshikamano.
Aidha, katika hatua nyingine Waziri Katambi amesisitiza raia wote wa kigeni wanaoingia nchini kufuata sheria na taratibu za nchi ili kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao.