Pambazuko FM Radio

Wazee Ifakara wanufaika na bima ya afya

3 October 2025, 9:56 am

Baadhi ya wazee waliopata kadi za bima ya CHF – Picha na; Isidory Mtunda

Wazee 300 na wajane 334 wa Ifakara wamepatiwa kadi za bima ya afya ya CHF ili kuboresha huduma za afya. Mkuu wa wilaya ameagiza maboresho ya huduma kwa wazee na kuwataka wawezeshwe mikopo ya asilimia 10.

Na; Isidory Mtunda

Wazee 300 na wajane 334 kutoka tarafa ya Ifakara, halmashauri ya mji wa Ifakara, wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, wamekabidhiwa kadi za bima ya afya ya CHF ili kupunguza changamoto wanazokutana nazo wanapotafuta huduma za afya.

Mkuu wa wilaya Kilombero katikati wakiwa katika picha ya pamoja na wazee wa tarafa ya Ifakara – Picha na Isidory Mtunda

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yaliyofanyika Oktoba 2, 2025 katika kijiji cha Kilama, mkurugenzi wa halmashauri Bi. Pili Kitwana alisema changamoto zilizowasilishwa na wazee ni pamoja na ukosefu wa bima za afya, upungufu wa dawa na rufaa zisizopatikana kwa wakati. Aliahidi kuwa halmashauri itazifanyia kazi kwa kushirikiana na wadau wa afya.

Mkurugenzi wa mji wa Ifakara, bi. Pili Kitwana ; Picha na; Isidory Mtunda
sauti bi. Pili Kitwana – mkurugenzi mji wa Ifakara

Kwa upande wao, wazee walioshiriki waliwasilisha risala iliyoeleza kuwa wengi wao hukosa dawa wanapofika katika vituo vya afya, hulazimika kununua dawa, na pia kukosa huduma ya rufaa wanapohitaji kuhamishiwa hospitali kubwa.

sauti ya msoma risala

Katika hatua nyingine Mgeni rasmi, mkuu wa wilaya wakili Dunstan Kyobya, ameagiza kuboreshwa kwa dirisha la wazee katika vituo vya afya na uchunguzi kufanyika kuhusu upungufu wa dawa. Pia alielekeza maafisa maendeleo ya jamii kuhakikisha wazee wanapata mikopo ya asilimia 10 kwa kuwa wana uwezo wa kufanya shughuli za uzalishaji ikiwemo kilimo na biashara.

sauti ya mkuu wa wilaya- Dunstan Kyobya