Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
11 September 2025, 7:56 pm

Ushahidi uliotolewa na Jamhuri ulithibitisha bila kuacha shaka.
Na Kuruthumu Mkata
Mahakama kuu iliyoketi Ifakara Kilombero imemhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa Elopi Kibolile Mwasuku (33) mkazi wa Kata ya Mchombe Halmashauri ya Mlimba baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka na kumuua mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mkusi mwenye umri wa miaka 14.
Hukumu hiyo imesomwa Septemba 9, 2025, mbele ya Jaji Steven Magoka, ambapo Mwendesha Mashtaka wa Serikali Dastan William alieleza kuwa tukio hilo lilitokea tarehe 29 Aprili, 2024 katika maeneo ya Mchombe.
Kwa mujibu wa upande wa Jamhuri, ushahidi uliwasilishwa na mashahidi 15, akiwemo daktari na mkemia wa serikali, ambao walithibitisha bila ya kuacha shaka kuwa mtuhumiwa alihusika moja kwa moja na tukio hilo la kikatili.
Baada ya kuridhishwa na ushahidi huo, mahakama ilimtia hatiani Elopi Mwasuku na kutoa adhabu ya kunyongwa hadi kufa, kwa mujibu wa sheria.