Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
4 June 2025, 1:22 pm

Maadhimisho ya siku ya mazingira ni nafasi nzuri ya kuhamasisha wananchi kuendelea kuchukua hatua madhubuti katika kudhibiti taka za plastiki na kuchangia katika ulinzi wa mazingira ya dunia nzima
Na Katalina Liombechi
Katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara, jamii imekuwa ikichukua hatua muhimu katika kudhibiti taka za plastiki licha ya changamoto za kiafya zinazoweza kujitokeza kwa wanaokusanya taka hizo kufanya shughuli hiyo bila ya kuwa na vifaa maalumu vya kinga.
Hizi ni juhudi ambazo zinahusisha sehemu kubwa ya wananchi ikiwa ni sehemu ya kuendelea kudumisha usafi wa mazingira na kudhibiti madhara yanayoweza kutokea kutokana na taka za plastiki.
Baadhi ya wananchi wanaokusanya taka hizo akiwemo Hamisa Said,Amos Gerard wamesema kuwa wanajivunia mchango wao kuweka mazingira katika hali ya usafi,kunufaika kiuchumi licha ya kueleza wasiwasi wao huenda wakakumbwa na magonjwa yanayotokana na uchafu kwani wengi wao hawana vifaa vya kinga kama vile glavu au maski hasa wanapopita katika maeneo hatarishi.

Meneja wa kiwanda kidogo cha kuchakata taka, kilichopo katika eneo la Maendeleo Mkuyuni Mahoso amesema kuwa licha ya changamoto zilizopo, kiwanda hicho kimeendelea kutoa mchango mkubwa katika kutunza mazingira kwani Kiwanda hiki kinachakata taka za plastiki na kuzipeleka katika viwanda vikubwa kwa ajili ya kuzigeuza kuwa bidhaa nyingine zinazoweza kutumika tena jambo ambalo linasaidia kupunguza mzigo wa taka katika mji wa Ifakara.

Afisa Afya wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara Bwana Jafari Ngogomela akizungumza na Pambazuko FM kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambapo amesema kuwa Halmashauri hiyo inatambua mchango mkubwa wa wananchi na viwanda vidogo vilivyopo kwa jitihada za kudhibiti taka za plastiki huku akieleza kuwa Halmashauri inaendelea kuimarisha mikakati ya kudhibiti taka za plastiki kwa kutoa elimu ya usafi wa mazingira, kutekeleza sheria ndogondogo zinazohusu usimamizi wa taka, na kuhamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za usafi wa mazingira.

Maadhimisho ya Siku ya mazingira katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara kwa mwaka huu 2025 yanatarajiwa kufanyika katika Mtaa wa Uhuru kata ya Ifakara ambapo kauli mbiu ya mwaka huu inasema “Mazingira yetu na Tanzania ijayo tuwajibike, dhibiti matumizi ya plastiki”.